Filamu ya “The sleepover”: Watoto wanavyofumbua mafumbo ya wazazi wao
- Ni filamu inayohusu watoto wanaoanza safari ya kuwaokoa wazazi wao waliotekwa.
- Kwa kuwa wanaifahamu familia yao vizuri, wanafumbua mafumbo yote yaliyoachwa na mama yao ili wamrudishe nyumbani.
- Huenda watoto hao pamoja na baba yao hawakujua kazi halisi ya mama yao.
Dar es Salaam. Imezoeleka wazazi huanza safari za kuwaokoa watoto wao lakini kwa filamu ya “The Sleepover”, hali ni tofauti.
Kundi la watoto wanne wanaanza safari kuwatafuta mama na baba yao ambaye wanaamini “ametekwa na maninja”.
Watoto hao akiwemo Lucy Forester (Dalila Bela) na Clancy Finch (Sadie Stanley) wanaongozana na wadogo zao Jackson Christison na Lucas Jaye huku wakilazimika kufumbua mafumbo yote ambayo mama yao amewaachia kama njia ya kumpata.
Wazazi wao hawakutekwa bure. Yote hayo yalianza hivi;
Margot Finch (mama yao) anatishiwa kuungana na wenzake ambao walikuwa wakifanya nao ujambazi kabla hajaanzisha familia yake. Kazi anayotakiwa kuikamilisha ni kuiba taji (crown) inayotajwa kuwa na gharama kubwa katika moja ya hafla ambayo wanatakiwa kuingia kama wageni waalikwa.
Zinazohusiana
- Project Power: Filamu mpya ya Netflix itakayoingia sokoni Agosti 14
- Filamu ya Fatal Affair: Kiboko kwa wachepukaji
- “Desperados”: filamu mahususi kwa wanaoteswa na mapenzi
Finch ambaye kwa sasa ameolewa na Glen Finch (baba) analazimika kufanya kazi na mpenzi wake wa zamani (Joe Manganiello) kuiba taji hilo.
Balaa linazidi kuwa zito pale watoto hao wanapooanza kugundua siri ambazo mama yao hakuwaambia.
Baba ambaye mbali na kuharibu mipango yote kwa kutokuwa na kitete na kihumwe humwe yupo njia panda akiwa haelewi ni kwanini yeye na mke wake wametekwa huku kichwa chake kikijaa maswali mengi ya ukweli kuhusu mke wake kabla hajamuoa na kuanzisha familia.
“Ukileta taji hilo, hakuna atakayeumia,” ni maneno ya Enuka Okuma ambaye amewateka wazazi hao.
Mbavu zako zina muda gani hazijaumia kwa kucheka? Kwa wapenzi wa komedi za familia, hii ni kati ya filamu zinazoweza kukufaa ukiwa kwenye wikiendi yako au baada ya kazi ngumu ya siku.
Hata hivyo, utahitaji kusubiri kwa sababu filamu hiyo itakuwa tayari katika mtandao wa Netflix ifikapo Agosti 21. Unaweza kuitazama kwa kupitia mtandao wa Netflix endapo umelipia kifurushi chako.
Kwa maelezo juu ya vifurushi, soma hapa.
Latest