Filamu ya “Royal Tour” haina maana tusipolinda vivutio vya utalii-Naibu Waziri

May 14, 2022 7:30 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Watanzania watakiwa kulinda na kuendeleza vivutio vya utalii.
  • Itasaidia kuvutia watalii wengi nchini.

Dar es Salaam. Wakati kampeni za kuitangaza filamu ya ‘The Royal Tour’ zikiendelea, Watanzania wametakiwa kushirikiana na kulinda na kuendeleza vivutio vya utalii ili kuipa maana filamu hiyo wageni wanapotembelea Tanzania.

Filamu hiyo  iliyorekodiwa kwenye hifadhi mbalimbali za Taifa na Mji Mkongwe huko Zanzibar ina lengo la kutangaza duniani vivutio vya utalii na uwekezaji vinavyopatikana hapa nchini.

Imetengenezwa chini ya wongozaji maarufu wa filamu duniani, Peter Greenberg ambaye wa kuirekodi aliambatana na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha wageni vivutio mbalimbali vya utalii, uwekezaji, sanaa na utamaduni vilivyopo nchini.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma Mkomi amewataka maafisa na askari wa uhifadhi waliohitimu mafunzo ya kijeshi kuhakikisha wanalinda vivutio vya utalii vilivyopo nchini kwa sababu filamu ya ‘The Royal Tour’ iliyozinduliwa hivi karibuni na Rais Samia haitakuwa na maana kama vivutio hivyo havitalindwa.

 “Filamu ile imezinduliwa  kwa lengo la kuhamasisha shughuli za utalii na uwekezaji nchini na tangu izinduliwe kila Mtanzania na dunia wanafahamu  Tanzania kuna nini,” amesema Mkomi Mei 13, 2022 alipokuwa akifunga mafunzo ya kijeshi kwa maafisa na askari 190 wa wizara hiyo.

Amesema mafunzo hayo yakawe chachu ya kuimarisha sekta ya utalii na  kuhakikisha watalii wanapata huduma katika mazingira bora ili kuwavutia zaidi kutembelea vivutio vilivyopo nchini.

Amewaeleza  wahitimu hao kuwa  wana wajibu wa kulinda misitu, wanyamapori, malikale na vyote ambavyo vinawavutia watalii kuja kutembelea.

“Niwaombe wahitimu mkatanguliza mbele uzalendo kwa kuhifadhi na kulinda vivutio vyote vya utalii vitakavyokuwa chini yenu, msipotoa huduma nzuri kwa watalii Filamu ya “Royal Tour” haitakuwa na maana yoyote” amesisitiza Naibu Katibu Mkuu.


Zinazohusiana: 


Mafunzo hayo yametolewa kwa maafis kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS),Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorogoro (NCAA) na Mamlaka ya Uhifadhi Wanyamapori Tanzania (TAWA). 

Mratibu wa Jeshi la Uhifadhi, Fidelis Kapalata amesema mafunzo hayo waliyoyapata katika yanakwenda kubadili mfumo wao kufanya kazi hususan katika kipindi hiki ambacho ujio wa watalii utakuwa mkubwa kufuatia kuzinduliwa kwa Filamu maarufu ya Royal Tour

Mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi TFS, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia – Utawala (SACC-Admn), Erasto Luoga anasema ni matarajio ya TFS baada ya mafunzo hayo wahitimu watakwenda kuishi utamaduni wa kijeshi na kuongeza kasi, ufanisi na uzalendo katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi wa rasilimali za nchi.

“Niipongeze Wizaya ya Maliasili na Utalii kwa kuratibu mafunzo haya yenye lengo la kubadirisha mfumo wa utendaji toka ule wa kiraia na kuwa wakijeshi, sasa taasisi zote za wizara zinakuwa na mfumo mmoja wa kijeshi ambao utasaidia katika mabadiliko ya kiutendaji,” amesema Luoga.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW