Famba: Polisi hawajawahi kuonya utapeli barakoa zenye kemikali
- Taarifa kuwa polisi wameonya uwepo wa wahalifu wanaotapeli kwa barakoa zenye kemikali ni uzushi.
- Polisi wasema hawajatoa tamko lolote kuhusu uvaaji wa barakoa kwa umma hivi karibuni.
Dar es Salaam. Iwapo wewe ni miongoni mwa watu waliopokea ujumbe unaodai Jeshi la Polisi limewaonya watu wasipokee barakoa zenye kemikali zinazogawiwa mtaani ili kujikinga na ugonjwa wa virusi vya Corona, acha kupoteza muda wako kuisambaza, ni uzushi.
Taarifa hiyo ambayo inaidaiwa imetolewa na jeshi hilo inatoa onyo kwa watu hasa waliopo majumbani kutokupokea barakoa kwa watu wasio wajua kwa sababu zina kemikali ambazo zinasababisha kupoteza fahamu.
Kwa sasa taarifa hiyo inayosambaa kwenye mtandao wa WhatsApp inaeleza zaidi kuwa hiyo ni mbinu ya wahalifu kuwapumbaza watu na kuwaibia vitu nyumbani.
Hata hivyo, taarifa hiyo imejaa mashaka mengi ambayo yanathibitisha kuwa haijatolewa na Jeshi la Polisi na ni uzushi mtupu unaolenga kuibua taharuki kwenye jamii wakati huu Serikali ya Tanzania ikikabiliana na COVID-19.
Ukweli uko wapi?
Taarifa hiyo haina ukweli wowote kwa sababu Jeshi la Polisi limesema halijatoa tamko lolote linalohusiana na suala hilo katika mitandao ya kijamii kwa sababu wana njia rasmi za kutoa taarifa.
“Sisi polisi hatutoi taarifa kwa namna hiyo. Kama tunatoa taarifa tunaita waandishi wa habari au tunaandika taarifa tunaituma kwenye vyombo vya habari ikiwa kwenye mfumo wa barua au sauti,” Msemaji wa jeshi hilo David Misime ameiambia NuktaFakti.
Misime amesema kama taarifa waliyotoa iko kwenye mfumo wa barua inakuwa na nembo ya Jeshi la Polisi na jina la ofisa aliyeitoa na inatumwa kupitia vyanzo vyao vya habari.
“Kwa hiyo taarifa, sisi kama Jeshi la Polisi hatujaitoa. Huyo aliyetengeneza ana nia yake mbaya kwa sababu taarifa yenyewe inaonekana kama inataka kutisha wananchi,” amesema.Hadi sasa,
Misime amesema polisi hawajapokea taarifa yoyote ya wahalifu kutumia barakoa zenye kemikali kuwadhuru watu ili wawaibie mali zao. Amewataka wananchi kufuata maelekezo ya Serikali kuhusu kuchukua tahadhari dhidi ya Corona ikiwemo kuvaa barakoa.
Zinazohusiana.
- Picha za tetemeko Croatia zilivyotumika kupotosha Corona mtandaoni
- Siyo kweli wananchi Italia wanatupa pesa mitaani kuepuka Corona
Mashaka mengine kuhusu taarifa hiyo
Jambo lingine linalotia mashaka katika taarifa hiyo ni kuwepo kwa makosa mengi ya uandishi katika taarifa hiyo ikiwemo lugha na kukosewa kwa baadhi ya herufi.
Kwa taasisi inayoheshimika kama polisi haiwezi kutoa ujumbe tata na wenye makosa lukuki.
Kwa vigezo hivyo taarifa hiyo ni uongo na inatakiwa kupuuzwa.