Faida za kupangilia chumba chako vizuri
- Utaokoa muda ambao unautumia kutafuta vitu au nguo zako.
- Ni hatua moja wapo ya usafi na itakuepusha na mafua.
- Itakupatia amani na utajisikia vizuri kuwa kwenye sehemu unayotumia kulala.
Dar es Salaam. Licha ya kuwa bado una hewa ya kuvuta na mkono unaenda kinywani, ni muhimu kufahamu kuwa zipo faida za kupangilia chumba chako na sehemu unapoishi.
Safari yangu ilikuwa hivi… Awali, kama ungepata nafasi ya kuingia chumbani kwangu, huenda ungedhani ni ardhi ya vita au mtu katoka kufumaniwa.
Hakukuwa na kitu kilichokuwa sehemu yake, licha ya kabati la nguo kuwepo, stendi ya viatu na hata kikapu cha nguo chafu.
Baada ya kusoma maandiko ya mwandishi wa masula ya maisha Mehwish Wahid katika tovuti ya Lifehack nilitafuta muda na kusafisha chumba changu na kubuni mambo kadha wa kadha kukiboresha. Ni geto hivyo hauhitaji kutegemea mengi. Haha, natania lakini haya ndiyo niliyofaidika nayo.
Utaokoa muda mwingi
Ni kweli, kabla ya kukipangilia chumba changu, nilikuwa nikihangaika kutafuta nguo niliyotaka kuivaa kwa muda mwingi sana. Kuja kuipata hiyo suruali, huenda hata jasho limenitoka. Hiyo ni suruali bado shati na mengineyo.
Tangu nipangilie, haichukui hata dakika kupata nguo ninayoitaka. Zaidi, hata nikidondosha kitu, ninajua pa kuangalia kwani najua hakijachangamana na nguo ambazo awali zilikua sakafuni.
Sitaki nikulishe maneno yangu pekee. Napenda usikie na wengine wanasemaje.
Usumbufu wa kutafuta nguo yako au kitu kwa muda mrefu utapungua utakapopanga chumba chako. Picha| Giphy.
Utaruhusu mzunguko wa hewa na utajisikia kuwa na amani
Kwenye harakati zangu, niliwahi kukutana na kijana obeid Moses almaarufu kama Santana ambaye ni mwanamuziki na mpiga vyombo vya muziki vikiwemo kinanda na gitaa jijini Dar es Salaam.
Nilienda nyumbani kwake kufanya mazoezi ya muziki na nilipoingia chumbani kwake, nilikuta kila kitu kiko kwenye nafasi yake. Kumbukumbu hiyo imenifanya nimuulize kwanini anapangilia chumba chake.
Santana amesema mbali na kuwa anatumia muda wake mwingi chumbani mwake na hivyo kumlazimu apaweke safi, amedadavua kuwa kwa kupanga chumba chake inampatia amani ya moyo.
“Ukiwa kwenye chumba chako kama ni kisafi unajisikia vizuri. Chumba chako ukikipangilia vilivyo, inakupatia mtazamo mzuri hata kwa wageni wako,” amesema Santana ambaye pia ni mwalimu wa vifaa vya muziki.
Utafahamu mali zako
Kama nguo zako zipo kila mahali na kila kona ya chumba unaweza kujihisi wewe ni tajiri wa mavazi. Lakini ukipangilia unaweza kushanga hata ndoo haujazi.
Kupitia kupangilia chumba chako, ni raisi kwako kuzifahamu mali zako na ni kipi unahitaji kununua kwa wakati husika.
Zinazohusiana
- Njia za asili zitakazokusaidia kukabiliana na tatizo la kukosa usingizi
- Jinsi ya kubaini kamera zilizofichwa kwenye nyumba ya kupanga, chumba cha hoteli
- Kwanini ukague usafi wa chumba cha hoteli kabla ya kutumia?
Kupunguza uwezekano wa kuvamiwa na wanyama na wadudu
Mwanafunzi wa udaktari kutoka Chuo cha Kikuu cha Kumbukizi ya Hubert Kairuki (HKMU) na mtengeneza maudhui ya dansi kwenye Instagram Hilary Henry amesema ukipangilia chumba chako ni lazima utafanya usafi na hivyo unaweza kuondoa wageni hao ambao hawahitajiki.
Hakika hauhitaji viumbe hao kukuaibisha na kukutia hasara ya kununua nguo mpya baada ya kuwa wamekutafunia zile ulizonazo.
Itakuboreshea afya yako
Witness Susuma ambaye ni mkazi wa Morogoro amesema kwake vumbi kidogo humfanya apate mafua makali na hivyo usafi wake kuwa salama ya afya yake.
Amesema “Nisiposafisha tu chumba ujue lazima nipate mafua. Nitadeki na nitapangilia vitu vyangu. Ni lazima nijali afya yangu.”
Wewe unamaoni gani juu ya usafi wa chumba chako? Acha maoni yako kwenye mitandao yetu ya kijamii.