Faida, hatari za uzazi njia ya upasuaji kwa wanawake Tanzania
- Mikoa ya Njombe, Kilimanjaro na Dar es Salaam yaongoza kwa idadi ya wanawake wanaozaa kwa upasuaji.
- Kuongezeka kwa vituo vya afya, vifaa vya kiteknolojia pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii vyatajwa kama sababu.
- Kupoteza damu nyingi na kuuguza kidonda muda mrefu ni miongoni mwa madhara.
Dar es Salaam. Tafiti zimebainisha kuwa kumekuwa na ongezeko la wanawake wanaojifungua kwa njia ya upasuaji (Cesarean section) kuliko ile ya kawaida huku mabadiliko ya sayansi na teknolojia yakitajwa kuchangia.
Ripoti mpya ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania (THDS-MIS) kwa mwaka 2022 inaonesha kujifungua kwa njia ya upasuaji kumeongezeka kwa asilimia nne ndani ya miaka 9.
“Asilimia ya watoto waliozaliwa wakiwa hai kwa njia ya upasuaji imeongezeka kutoka asilimia 7 katika utafiti uliofanyika mwaka 2015–16 hadi asilimia 11 katika utafiti wa TDHS-MIS wa mwaka 2022,” imesema ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imefafanua kuwa asilimia hizo ni za wale waliozaliwa wakiwa hai hata kama ni kwa muda au siku chache.
‘Caesarean section’ ni aina ya uzazi inayohusisha kulipasua tumbo la uzazi la mama na kumtoa mtoto. Njia hii inaweza kuwa ya hiari au ya lazima.
Soma zaidi : Utafiti:Zaidi ya watanzania milioni sita hawatumii vyoo
Njia ya hiari ni ile ambayo mama huomba kufanyiwa kutokana na sababu mbalimbali za kiafya au maamuzi ya familia huku njia ya dharura ikitumika zaidi wakati mama akipata matatizo wakati akijifungua kwa njia ya kawaida.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) njia hi ya uzazi imekuwa iliyotumika sana katika siku za hivi karibuni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo maendeleo katika sekta ya afya.
“Duniani kote viwango vya upasuaji wakati wa kujifungua vimeongezeka kati ya asilimia saba mwaka 1990 hadi asilimia 21 hivi karibuni na inakaridiwa kuongezeka katika karne ya hivi karibuni,” imesema WHO katika taarifa yake iliyotolewa Juni 21, 2023.
Wakati WHO ikionesha kuongezeka kwa viwango vya upasuaji duniani, ripoti ya THDS-MIS inasema aina hiyo ya upasuaji nchini Tanzania kwa mwaka 2022 ilifanyika zaidi katika hospitali binafsi kuliko zile za Umma.
“Asilimia ya watoto waliozaliwa wakiwa hai katika vituo vya afya vinavyomilikiwa na watu binafsi ni 30, ikifuatiwa na zile za kidini asilimia 28. Vituo vya afya vya Umma vina asilimia 12 ikiwa ndio ya chini zaidi,” imesema ripoti hiyo.
Miongoni mwa faida za kujifungua kwa upasuaji ni pamoja na kuokoa maisha ya mama na mtoto kepuka maumivu ya uchungu wakati wa kujifungua pamoja na kupunguza kuvuja damu. PichalNews Medical
Kwanini uzazi kwa njia ya upasuaji unaongezeka?
Daktari Living Kimaro, kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili ameiambia Nukta Habari kuwa kuongezeka kwa vituo vya afya, vifaa vya kiteknolojia pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii ndio chanzo cha kuongezeka kwa njia ya uzazi kwa upasuaji.
“Serikali imeongeza vituo vya afya, wameongeza theatre(chumba cha upasuaji) lengo likiwa ni kupunguza vifo vya mama na mtoto hivyo kuongeza idadi ya wanaofanyiwa upasuaji…
…Sasa hivi pia kuna mambo ya mitandao ya kijamii unakuta wazazi watarajiwa wanaangalia wengine wanavyojifungua kwa njia ya kawaida ‘YouTube’ wanaingiwa hofu na kutamani kuzaa kwa upasuaji,” ameongeza Dkt. Kimaro.
Kwa mujibu wa kitabu cha hali ya uchumi kwa mwaka 2022, Tanzania ina jumla ya vituo vya afya vinavyofanya kazi 11,041 ukilinganisha na vituo 10,153 vilivyokuwepo mwaka 2021.
Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 8.7 huku vituo 6,682 sawa na asilimia 60.5 vikimilikiwa na Serikali, vituo 3,318 (asilimia 30.1) vikimilikiwa na sekta binafsi pamoja na vituo 1,041 sawa na asilimia 9.4 vinavyomilikiwa na mashirika ya dini.
Soma zaidi:‘Betting’, vinywaji baridi kuchangia bima ya afya kwa wote Tanzania
Faida, hatari zake
Licha ya umuhimu wa uzazi kwa njia ya upasuaji, WHO imebainisha na hatari wanazoweza kukutana nazo wajawazito baada ya kujifungua ikiwemo kuuguza vidonda kwa muda mrefu, kuvuja damu uwezekano wa kupata matatizo katika mimba nyingine zitakazokuja.
“Kama ilivyo kwa aina nyingine za upasuaji, kunaweza kutokea hatari ikiwemo ucheleweshaji wa kuanza kunyonyesha na kuongezeka kwa uwezekano wa matatizo katika mimba ya baadaye,” imesema WHO.
Daktari Kimaro amesema miongoni mwa faida za kujifungua kwa upasuaji ni pamoja na kuokoa maisha ya mama na mtoto kepuka maumivu ya uchungu wakati wa kujifungua pamoja na kupunguza kuvuja damu.
“Faida za kuzaa kwa oparesheni(upasuaji) ni kuokoa maisha ya mama na mtoto na umwagikaji damu wakati wa kujifungua” ameongeza Daktari Kimaro.
Aidha, Daktari huyo amewashauri wajawazito kutokuogopa kutumia njia ya upasuaji wakati wa kujifungua kwani ikitumika kwa usahihi inaweza kuwahakikishia usalama wa maisha yao pamoja na watoto.
Soma zaidi: Mwandishi wa Nukta Africa ashinda tuzo ya takwimu ya NBS 2023
Njombe kinara wa ‘Caesarean section’
Licha ya mkoa wa Njombe kuwa miongoni mwa mikoa yenye idadi ndogo ya watu, ripoti ya THDS-MIS inasema kuwa mkoa huo umeongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanawake wanaofanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua kwa asilimia 33.
Hiyo inamaamnisha katika kila wanawake 10 wanaojifungua mkoani humo watatu walifanyiwa upasuaji.
Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 mkoa wa njombe una watu 889,946 kati yao wanawake ni 420,533 na wanaume ni 469,413.
Idadi hiyo ya wanawake waliojifungua kwa upasuaji imeongezeka kwa asilimia 19.3 kutoka asilimia 13.7 iliyokuwepo mwaka 2015-2016.
Ingawa mkoa huo unaongoza kwa asilimia kubwa ya wanawake kujifungua kwa upasuaji, bado una idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa kwa njia hiyo.
Kwa mwaka 2022 walikuwa 47 sawa na asilimia 1.07 ya watoto wote 4,735 waliozaliwa kwa njia ya upasuaji mwaka 2022.
Mbali na mkoa wa Njombe, mikoa mingine iliyoongoza kwa kujifungua kwa upasuaji ni pamoja na mkoa wa Kilimanjaro wenye asilimia 30 ya watoto waliozaliwa kwa upasuaji sawa na watoto 107.
Mkoa wa Dar es Salaam unaoongoza kwa idadi ya watu nchini ulikuwa na jumla ya watoto 104 waolizaliwa kwa upasuaji sawa na asilimia 26 ikifuatiwa na mikoa wa Ruvuma na Iringa yenye asilimia 23 za watoto waliozaliwa kwa upasuaji.