Facebook kuwakutanisha watumiaji wake kwenye ‘vyumba’ maalum

April 25, 2020 9:31 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni vyumba vya kidijitali vinavyowawezesha kuchati na kuonana wakiwa mbali. 
  • Vyumba hivyo vitasaidia kuimarisha mahusiano ya watu wakati huo wa janga la Corona. 
  • Vyumba hivyo pia vitaanza kutumika WhatsApp na Instagram hivi karibuni. 

Dar es Salaam. Licha ya janga la Corona (COVID-19) kupunguza ukaribu wa watu kuonana uso kwa uso, kampuni za teknolojia zinaendelea na juhudi kutumia changamoto hiyo kama fursa ya kuwaunganisha watu kidijitali ili kuimarisha mahusiano yao ya kazi, urafiki na undugu. 

Mtandao wa kijamii wa Facebook umetangaza kuongeza baadhi ya vipengele katika bidhaa zake za Messenger na Facebook ili kuwezesha mazungumzo kwa njia ya video kuwa rahisi na yenye ufanisi mkubwa kwa watumiaji wa mtandao huo. 

Miongoni mwa vipengele vilivyoongezwa ni “Messenger Rooms” au (vyumba katika programu ya Messenger) ambavyo ni makundi yanaruhusu watu kupigiana simu za video na kuonana mubashara hata kama wako mbali. 

“Watumiaji wanaweza kuunda chumba kwenye Messenger au Facebook na kumwalika mtu yoyote hata kama hana akaunti ya Facebook. Vyumba hivyo vitaweza kubeba watu hadi 50 kwa wakati mmoja,” inaeleza sehemu ya taarifa ya Facebook iliyotolewa jana usiku (Aprili 24, 2020)

Muonekano wa Messenger Rooms kwenye simu na kompyuta. Picha|Facebook. 

Kwa kutumia Messenger Rooms, watumiaji wa mtandao huo wanaweza kuendesha tukio lolote la sherehe, klabu ya vitabu au hata kuchati na kubadilishana mawazo na ndugu, marafiki au wafanyakazi. 

Pia wanaweza kutuma mialiko hiyo kwenye makundi na matukio mbalimbali ya Facebook, jambo litakalowasaidia kuondokana na upweke na msongo wa mawazo.  

Facebook imesema hivi karibuni huduma hiyo itaanza pia kutumika Instagram na WhatsApp ambako mazungumzo kwa njia ya video hayahusishi watu wengi kwa wakati mmoja. 

“Simu za video za WhatsApp ni njia nyingine ya kukutana. Muda si mrefu watumiaji wanaweza kuwa na mazungumzo ya sauti na video ya watu hadi nane kwa wakati mmoja,” imeeleza taarifa hiyo. 

Baada ya mtumiaji kutengeneza chumba chake cha maongezi, anaweza kuchagua nani aone, kujiunga na kumuondoa mtu yeyote kwenye mazungumzo kadiri atakavyoona inafaa. 


Zinazohusiana: 


Hata hivyo, Facebook imesema ili kuhakikisha usalama unakuwepo kwenye vyumba hivyo, imetengeneza sera za usiri na faragha na kabla ya kuanza kutumika itafanya majaribio katika baadhi ya nchi ili kuona kama kipengele hicho kinafaa wakati huu wa Corona.  

Baadhi ya watumiaji wa Facebook wameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa huenda mabadiliko hayo yakawasaidia kuimarisha mahusiano yao hasa kipindi hiki ambacho hawawezi kuona ana kwa ana kutoka tahadhari ya ugonjwa wa COVID-19. 

“Ni hatua nzuri kwa Facebook kuwajali na kuwatafutia njia mbadala ya kuwasiliana watumiaji wake lakini intaneti itakuwa changamoto kwa wengi kwa sababu mazungumzo ya video yanatumia bando la intaneti sana,” amesema Nicodemus Kakote, mkazi wa jijini Dar es Salaam.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW