Facebook kujisafisha kwa Sh6.9 trilioni

April 25, 2019 8:12 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Licha ya Facebook kupitia misukosuko mingi bado unatamba katika biashara ya mitandao ya kijamii duniani. Picha|Mtandao.


  • Mtandao huo umetenga kiasi hicho cha fedha ili kujiandaa kulipa faini ya kujihusisha katika vitendo vya matumizi mabaya ya data za watumiaji wake. 
  • Kashafa hiyo ni ile ya kampuni ya Cambridge Analytica ya Uingereza  iliyotumia data za watumiaji wa Facebook takribani 87 milioni kwa madhumuni ya kibiashara na kisiasa. 

Mtandao wa Facebook umetenga Dola za Marekani 3 bilioni (Sh6.9 trilioni) ikiwa ni hatua ya kujiandaa kulipa faini baada ya kuhusika katika vitendo vya kuhujumu faragha na kuvujisha taarifa za watumiaji wa mtandao huo. 

Mtandao huo umesema jana (Aprili 24, 2019) kuwa umetenga kiasi hicho cha fedha kutokana na uchunguzi unaoendelea wa Tume ya Shirikisho la Biashara ya Marekani (FTC) unaohusiana na tuhuma za matumizi mabaya ya taarifa za watumiaji wa mtandao wa Facebook. 

FTC bado haijatangaza kiasi cha fedha ambacho Facebook itatakiwa kulipa, lakini mtandao huo umesema faini hiyo inaweza kufikia Dola za Marekani 5 bilioni (Sh11.5  trilioni), ambacho kitakuwa kiasi kikubwa zaidi cha faini kwa kampuni ya teknolojia kutozwa duniani. 

Uchunguzi wa FTC umejikita katika kubaini kama kampuni hiyo ilikiuka sera ya faragha ikiwemo kuvunja makubaliano ya kutunza taarifa binafsi za watumiaji wake. 

Tume hiyo inayosimamia haki za walaji ilianza uchunguzi wake baada ya kuibuliwa kwa kashfa mwaka 2018 ya kampuni ya Cambridge Analytica ya Uingereza  iliyotumia data za watumiaji wa Facebook takribani 87 milioni kwa madhumuni ya kibiashara na kisiasa.  


Zinazohusiana: 


Hata hivyo, bado skendo hizo hazijaiyumbisha Facebook kwa sababu  watumiaji na matangazo yanaendelea kutangazwa. 

Katika robo ya kwanza ya mwaka 2019 mtandao huo ulipata zaidi ya matarajio ya Dola za Marekani 15.08 bilioni (Sh11.7 bilioni) katika mauzo na idadi ya watumiaji wake inaongezeka kwa asilimia nane kila mwezi hadi sasa ina  watumiaji zaidi 2.38 bilioni.

Mchambuzi kutoka kampuni ya eMarket, Debra Aho Williamson amesema Facebook itabaki kuwa ni sehemu sahihi ya kutangazia huduma na bidhaa ili kuwafikia watu wengi licha ya matatizo yanayoikumba kampuni hiyo. 

“Watu wa matangazo wanaendelea kushikamana na Facebook, licha ya changamoto nyingi,” amesema na kuongeza kuwa, “Wanachojali zaidi ni watumiaji, uwezo wake na wote wanazidi kuonyesha utendaji mzuri.”

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW