ESG: Vodacom Tanzania yapunguza 24% ya hewa chafu
- Sehemu ya mafanikio hayo imetokana na kubadilisha vifaa vya zamani vya mawasiliano ya redio katika maeneo 1,808 ndani ya miezi saba.
Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania Plc imepunguza uzalishaji wa hewa chafu kwa asilimia 24 katika mwaka wa fedha ulioishia Machi 31, 2026, huku ikiongeza uwekezaji katika ufanisi wa matumizi ya nishati na uboreshaji wa miundombinu ya mtandao.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Mazingira, Jamii na Utawala (ESG) ya kampuni hiyo iliyozinduliwa hivi karibuni uzalishaji wa hewa chafu ulipungua kutoka tani 24,285.6 hadi tani 18,445.5 katika kipindi hicho.
Upunguzaji wa hewa chafu ni miongoni mwa masuala ya kimazingira yanayopigiwa upatu zaidi ulimwenguni katika uendeshaji wa taasisi ili kulinda mazingira na kuifanya dunia iwe salama kuishi.
Vodacom imesema kupungua huko kulienda sambamba na kushuka kwa matumizi ya dizeli kwa asilimia 24, kutoka lita milioni 8.6 mwaka 2025 hadi lita milioni 6.6 mwaka ulioishia Machi 2026.

Dizeli na mafuta mengine ya petroli ni miongoni mwa nishati zinazochangia uchafuzi wa mazingira.
Ili kuboresha matumizi endelevu ya nishati, kampuni hiyo inayoongoza kwa idadi ya watumiaji nchini kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema imewekeza Sh3.5 bilioni katika hatua za kuongeza ufanisi wa matumizi ya nishati.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa kiasi cha fedha kilichowekezwa kinalenga kufikisha uokoaji wa megawati 18,340 mwaka huu, ikiwa zaidi ya mara sita ya megawati 2,861 zilizookolewa kwa mwaka wa 2025.
Uboreshaji miundombinu wachangia
Sehemu ya mafanikio hayo imetokana na kubadilisha vifaa vya zamani vya mawasiliano ya redio katika maeneo 1,808 ndani ya miezi saba, pamoja na kuongezeka kwa upatikanaji wa umeme wa gridi ya taifa uliopunguza utegemezi wa jenereta katika vituo vya data.
Kampuni hiyo imesema mtandao wake hutumia takriban gigawati-saa (GWh) 169.5 za nishati kwa mwaka katika maeneo zaidi ya 3,800, ambapo maeneo 2,190 yako vijijini. Vituo vya msingi vya mtandao vinatajwa kutumia asilimia 78.9 ya nishati hiyo.
Katika kipindi hicho, maeneo 169 yaliyokuwa nje ya gridi ya Taifa yaliunganishwa kwenye gridi, hatua ambayo kampuni inasema imechangia kupunguza matumizi ya mafuta.
Mfano, katika kituo cha data cha Kwale ambako upatikanaji wa umeme wa gridi uliongezeka kutoka 11 kVA hadi 33 kVA. Hatua hiyo ilipunguza matumizi ya jenereta kutoka saa 18 kwa siku hadi saa mbili, sawa na kupungua kwa asilimia 88 kwa matumizi ya dizeli katika kituo hicho.

Aidha, zaidi ya nusu au asilimia 57 ya nishati iliyotumiwa na Vodacom Tanzania ilitokana na vyanzo vya nishati jadidifu. Kampuni pia imesema imehuisha cheti chake cha ISO 50001 kinachohusiana na mifumo ya usimamizi wa nishati.
Uzalishaji wa hewa chafu unaohusishwa na shughuli za kampuni na mnyororo wake wa thamani nao ulipungua kutoka tani 100,455 hadi tani 94,944.
Mkurugenzi wa Miundombinu ya Mtandao wa Vodacom Tanzania, Andrew Lupembe, amesema hatua hizo zimekuwa na manufaa mawili kwa kampuni na wateja, ikiwamo kuboresha huduma huku ikipunguza matumizi ya mafuta.
“Mafanikio haya ya kimazingira yametokana na kufanya uhandisi wa msingi kwa usahihi, siyo kutoka mradi tofauti wa uendelevu,” amesema Lupembe.
Mtandao na huduma za kifedha
Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa huduma za mtandao wa 4G zilifikia asilimia 76.3 ya wakazi, huku wateja wa kampuni hiyo wakifikia milioni 27.7 baada ya uzinduzi wa huduma ya 5G.
Umiliki wa simu janja umefikia asilimia 46.7, huku wateja 325,415 wakipata vifaa kupitia ubia wa mikopo ya rejareja.
Kwa upande wa huduma za kifedha, M-Pesa imehudumia wateja milioni 14.1, huku M-Koba, jukwaa la kidijitali la vikundi vya akiba, likifikia vikundi hai 299,420. Akiba kupitia jukwaa hilo iliongezeka kwa asilimia 81 katika mwaka huo.
Katika kuimarisha huduma za kijamii, Vodacom Tanzania Foundation, taasisi isiyo ya kifaida ya kampuni hiyo, ilifikia wanufaika milioni 2.9 kupitia programu mbalimbali, ikiwamo ushirikiano na Taasisi ya Elimu Tanzania uliowezesha kuondolewa kwa gharama za data kwenye jukwaa la kitaifa la maendeleo ya walimu.
Kampuni hiyo imesema hatua hiyo iliwezesha walimu 121,832 kupata nyenzo za maendeleo ya kitaaluma bila gharama za data.
Katika eneo la mazingira, Vodacom imesema miti 80,000 ya asili imepandwa katika Msitu wa Kahe 2, eneo la Mlima Kilimanjaro.
Usalama kazini na data
Kwa upande wa usalama kazini, kampuni hiyo imesema imefikia mwaka wa 14 mfululizo bila kurekodi kifo cha mfanyakazi mahali pa kazi.
Mpango wa uboreshaji wa mtandao ulihusisha wafanyakazi 411 waliosafiri zaidi ya kilomita milioni 1.7, huku awamu ya kwanza ya mpango huo ikikamilika bila kifo au tukio kubwa la kiusalama, kwa mujibu wa kampuni.
Vodacom Tanzania pia imesema ina uthibitisho wa ISO 27001 kwa mifumo ya usalama wa taarifa na haikurekodi faini inayohusiana na ushindani usio halali au utakatishaji fedha katika kipindi kilichoripotiwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire, amesema kampuni yao itaendelea kuunganisha uwekezaji wa biashara na athari zake kwa jamii na mazingira.
“Nyuma ya kila muunganisho kuna maisha yanayobadilika, mwalimu anayefikia nyenzo za kujifunzia bila gharama ya data, kikundi cha akiba ambacho hakihifadhi tena fedha taslimu. Tutaendelea kuwajibika kwa wananchi wa Tanzania wanaotuamini kila siku,” amesema Besiimire.
ESG ni miongoni mwa masuala yanayokaguliwa kwa kina katika miaka ya karibuni ili kuhakikisha uendeshaji wa shughuli za taasisi zinachangia kuboresha maisha ya watumiaji na jamii kwa ujumla badala ya kuwazia faida pekee.