Elimu, mkaa mbadala kupungua ukataji miti ya asili

February 9, 2019 12:59 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali, sekta binafsi watakiwa kujielimisha zaidi juu ya matumizi ya mkaa ili kupata suluhisho la pamoja katika kutafuta nishati endelevu itakayosaidia kupunguza ukataji miti.
  • Baadhi ya wadau washauri msisitizo uwe katika matumizi ya mkaa mbadala na gesi ya majumbani. 

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema Serikali na taasisi binafsi wana kila sababu ya kuendelea kujifunza kuhusu matumizi ya mkaa ili kupata maarifa na ujuzi utakaosaidia kukabiliana na ukataji miti. 

Miti imekuwa ikutumika kutengeneza nishati ya kuni na mkaa inayohitajika katika shughuli mbalimbali za uzalishaji na matumizi ya majumbani lakini ni miongoni mwa vichocheo vikubwa vya uharibifu wa mazingira. 

Makamba aliyekuwa akizungumza katika mdahalo wa Jukwaa la Fikra kujadili matumizi ya mkaauliondaliwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) jana Februari 7 jijini hapa, amesema ni vema wadau wa mazingira na wananchi wakubali kuwa bado hawajui sana kuhusu mkaa na wajipe muda wa kutafakari ili kupata njia sahihi za kupunguza matumizi yake. 

“Inabidi tukubali kuwa hatujui sana kuhusu mkaa wote sekta binafsi na sisi Serikali. Tuna nafasi ya kujifunza zaidi hata wale wasomi ambao wanafanya tafiti bado tuna nafasi ya kuujua mkaa,” amesema Makamba. 

Amebainisha kuwa kumekuwa na dhana potofu katika jamii kuwa mkaa ni nafuu ukilinganisha na nishati zingine lakini gharama zake kwa mazingira, afya ya binadamu na uchumi wa nchi ni kubwa .

“Mkaa sio nafuu kwa sababu bei yake haipimwi kihalali, lakini pia sio nafuu maana unaathiri afya zetu. Tanzania ni mojawapo ya nchi tano Duniani inazoongoza kwa ukataji wa miti na misitu,” amesema aliungana na wadau mbalimbali kutafuta suluhisho la matumizi ya mkaa nchini ili kuokoa mazingira. 

Katika hatua nyingine, amesema sekta binafsi zikiwemo taasisi za elimu, uzalishaji bidhaa zishirikishwe kikamilifu katika kutumia mkaa mbadala ili kupunguza ukataji miti ya asili. 

Chuo Kikuu cha Dodoma kimeonyesha mfano katika matumizi ya mkaa mbadala chuoni hapo unaotumika kupikia chakula za wanafunzi takribani 27,000

“Sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kutafuta matumizi ya nishati mbadala,” amesema Makamba. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba akizungumza katika mdahalo wa Jukwaa la Fikra kujadili matumizi ya mkaa, uchumi na mazingira yetu, jijini Dar es Salaam jana.Picha|Mwananchi.  

Wadau mbalimbali nao wametoa mapendekezo yao yatakayosaidia kupunguza matumizi ya mkaa na kuhakikisha suluhisho la mkaa endelevu linapatikana ili kulinda misitu asili. 

Ofisa Misitu Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Charles Meshack amesema njia rahisi ni Serikali kuundaa sera ya kudhibiti matumizi ya mkaa kwasababu ni nishati inayowahusisha watu wengi na inatakiwa kuwa na usimamizi wa kisheria na kikanuni. 

Amesema kutokana na ongezeko la watu, kila siku miti 14,900 hukatwa na kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa basi hadi kufikia 2060 kutakuwa hakuna miti nchini. 

“Tunakata miti ya asili halafu tunapanda miti mipya, kupanda miti mipya siyo suluhisho kwasababu miti ya asili inajiotea yenyewe. Ni vema tuwe na miti ya kuvuna kwa mkaa endelevu,” amesema Meshack. 


Zinazohusiana:


Hivi karibuni Serikali ilitoa maagizo kuwa kila Wilaya nchini ihakikishe inapanda miti isiyopungua milioni moja kila mwaka. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Kuhifadhi Mazingira, Ali Mafuruki amesema njia pekee ya kupunguza ukataji miti ya asili ni kutumia mkaa wa mianzi kwasababu ni endelevu na inazaliana sana kwa muda mfupi. 

Amesema kwa hali ilivyo sasa ya ukataji miti, biashara ya mkaa siyo jambo la kuunga mkono. 

Hata hivyo, wazungumzaji wengine waliokuwepo katika mdahalo huo, wamesisitiza umuhimu wa Serikali kupunguza kodi ya gesi inayotumika majumbani ili kuongeza idadi ya watu wanaotumia nishati hiyo. 

Enable Notifications OK No thanks