Dk Mpango kukutana na vigogo wa Benki ya Dunia, IMF kujadili uchumi wa Tanzania

April 10, 2019 7:26 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Majadiliano  hayo yatajikita kwenye maeneo ya mwenendo wa uchumi wa dunia; miradi ya maendeleo iliyopendekezwa na Benki ya Dunia kwa mwaka 2019/20
  • Yatafanyika sambamba na mikutano ya kipupwe (Spring Meetings) ya taasisi hizo za fedha duniani inayofanyika Jijini Washington DC ambapo Dk Mpango anaongoza ujumbe wa Tanzania.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango atashiriki katika majadiliano na viongozi wa juu wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) wanaoshughulikia masuala ya Afrika kuhusu utekelezaji wa programu za sera za kiuchumi, mikopo nafuu na misaada ya kitaalam kwa Tanzania.

Majadiliano hayo yatafanyika sambamba na mikutano ya kipupwe (Spring Meetings) ya taasisi hizo za fedha duniani inayofanyika Jijini Washington DC, Marekani ambapo Dk Mpango ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mikutano hiyo. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango, majadiliano  hayo yatajikita kwenye maeneo ya mwenendo wa uchumi wa dunia; miradi ya maendeleo iliyopendekezwa na Benki ya Dunia kwa mwaka 2019/20

Pia kujenga uwezo wa rasilimali watu, mahitaji ya kujenga uchumi wa kidijitali na maeneo mengine ambayo Benki ya Dunia inaweza kusaidia kupatikana mikopo nafuu  ya kugharamia miradi ya kipaumbele hasa reli na umeme hapa nchini. 

“Waziri wa Fedha pia anatarajia kupata fursa ya kukutana na Taasisi na mashirika mbalimbali ya kimataifa, washirika wa maendeleo na wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo. 


Soma zaidi:


Akizungumza kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Jijini Washigton DC, Dk Mpango ameihakikishia jumuiya ya kimataifa na watanzania kwa ujumla kuwa Tanzania inafanya vizuri kiuchumi na kijamii na kumpongeza Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Wilson Masilingi kwa jitihada kubwa anazozifanya kuitangaza nchi na kusukuma mbele agenda za nchi.

Mikutano hiyo ya kipupwe inayofanyika Aprili 8-14, 2019 inatoa fursa kwa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka katika nchi wanachama ambao pia ni Magavana wa Benki ya Dunia na IMF kujadili maendeleo na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa masuala ya maendeleo na ushirikiano.

Pia hutoa fursa kwa nchi kushiriki kama mwanahisa kwenye mikutano ya kiutawala (Board of Governors) ya taasisi hizo mbili ambapo maamuzi ya kiuendeshaji na kisera hufanyika.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango (kushoto) akiteta jambo na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Balozi Wilson Masilingi wakati wa kikao cha maandalizi cha Ujumbe wa Tanzania kwenye Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kilichofanyika kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, Mjini Washington DC. Picha Wizara ya Fedha na Mipango.

Kwa Upande wake, Balozi wa Tanzania nchni Marekani, Wilson Masilingi akiukaribisha ujumbe wa Tanzania nchini Marekani amesema kuwa yeye na timu yake wamejipanga kuhakikisha ushiriki wa nchi katika mikutano hiyo unakuwa mzuri na wenye manufaa na mafanikio kwa Taifa.

Tanzania itapata pia fursa ya kushiriki katika Kamati Maalum za Benki ya Dunia na IMF na baadhi ya mikutano hiyo ni Mkutano wa Mawaziri wa Fedha inayoshughulikia sera na utulivu wa Sekta ya fedha (International Monetary Committee and Finance Committee-IMFC).

Enable Notifications OK No thanks