Dk Kigwangalla; Serikali haiwezi kulipa fidia kwa wananchi wanaovamiwa na wanyama pori

May 6, 2019 7:38 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla. Picha|Mtandao.


  • Amesema wataendelea kutoa kifuta machozi kwa sababu gharama zitakuwa kubwa na watashindwa kuwatunza wanyama hao. 
  • Amesema thamani ya mwanadamu anayeuwa na wanyama wakali hailingani na fidia itakayotolewa.
  • Amesema vifo vinavyotokea na uvamizi wa wanyama ni bahati mbaya. 

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amesema Serikali inaweza kuendelea kuwalipa kifuta machozi na siyo fidia wananchi wanaoishi karibu na hifadhi za Taifa wanaopata madhara yatokanayo na wanyama pori kuingia katika vijiji vyao. 

Dk Kigwangalla ametoa ufanunuzi huo bungeni leo (Mei 6, 2019) wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka aliyetaka kujua ni lini Serikali itakuja na marekebisho ya sheria ili badala ya kutoa kifuta machozi kwa wananchi hao wawe wanapata fidia inayotokana na uharibifu wa mazao ya mashambani. 

“Kusema serikali itaji committ (itajitoa) kulipa fidia ni jambo gumu kwa sababu gharama itakuwa kubwa sana na mwisho wa siku tutashindwa kutunza hizi maliasili ambazo sisi sote tunapaswa kuzilinda kwa mujibu wa Katiba ya Jumhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 27,” amesema Dk Kigwangalla. 

Amesema ugumu wa kutolipa fidia unatokana na ukweli kuwa sababu za wanyama hao kwenda katika vijiji vya wananchi ni nyingi na Serikali inaweza kulipa kifuta machozi na siyo fidia na kama itafanya hivyo itakuwa na mzigo mkubwa wa kuhifadhi wanyama pori. 

“Wakati mwingine wananchi wanafuata wanyama kwenye mapito yao, ama mazalia yao, ama maeneo ya mtawanyiko. Wakati mwingine sisi viongozi tukiwemo wabunge, madiwani tunahamasisha sana Serikali iweke maeneo ya hifadhi ambayo kiuhasili ni lazima yatapitiwa na wanyama,” amesema Kigwangalla.

Kwa sababu sisi tunaoishi karibu na hifadhi kumekuwa na uharibifu mkubwa wa mazao unaotokana na wanyama waharibifu kama tembo, nguruwe na wanyama wengine waharibifu. Serikali imekuwa ikitoa kitu kinachoitwa kifuta machozi, sasa ni lini Serikali itakuja na marekebisho ya sheria ili badala ya kutoa kifuta machozi wananchi hao wawe wanapata fidia inayotokana na uharibifu wa mazao ya mashambani.”- Zuberi Kuchauka.

Dk Kigwangalla ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Vijijini amebainisha kuwa uharibifu ikiwemo vifo vinavyotokea ni bahati mbaya, na hata Serikali ikitoa fidia haitalingana na thamani ya mwanadamu aliyepoteza maisha. 

Amewataka wabunge na wananchi wote watambue kwamba wanyama pori ni maliasili ya Taifa, ni utajiri, ni urithi wa Taifa letu na hawawezi kamwe kuacha kuilinda kwa ajili ya matumizi ya sasa na vizazi vijavyo.


Soma zaidi:


Kwa nyakati tofauti kumekuwa kukiripotiwa matukio ya wanyama pori kutoka katika hifadhi za Taifa na kuvamia mashamba na makazi ya wana vijiji wanaoishi karibu na maeneo hayo na kufanya uharibifu mkubwa. 

Mathalan, mwaka 2015 kundi la tembo takriban mia mbili walivamia makazi ya wananchi wa kijiji cha Nyamatoke kata ya Mosongo wilayani Serengeti mkoani Mara na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazao mashambani.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW