Dk Faustine Ndugulile afariki dunia nchini India
- Afariki ikiwa ni miezi mitatu tangu achanguliwe kuwa Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika.
Arusha. Arusha. Dk Faustine Ndugulile ambaye pia ni Mbunge wa Kigamboni (CCM) amefariki dunia leo Novemba 27, 2024 nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu ikiwa ni miezi mitatu tangu achaguliwe kuwa Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Taarifa ya Spika wa Bunge la Tanzania Dk Tulia Ackson iliyotolewa asubuhi ya leo Novemba 27, 2024 kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo instagram imethibitisha kifo cha mbunge huyu huku akitoa pole kwa wanafamilia, wabunge na wananchi wa jimbo la Kigamboni.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile. Kwa niaba ya Wabunge natoa pole kwa familia, wakazi wa Kigamboni na Watanzania wote. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi”, amesema.
Aidha, ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia imesema inaendelea kuratibu shughuli za mazishi na taarifa zaidi zitaendelela kutolewa.
Enzi za uhai wake Dk Ndugulile alipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika anga za kimataifa baada ya Agosti 27 mwaka huu kutangazwa mshindi katika zoezi la upigaji kura lililofanywa na nchi 19 kutafuta Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika.
Matokeo ya ushindi wake yalitangazwa usiku wa Agosti 27 mwaka huu katika mkutano wa afya uliofanyika Congo Brazzaville.
Baada ya ushindi huo Dk Ndugulile alipewa miezi sita ya kuandaa mpango kazi kabla ya kuanza majukumu yake mapya mwezi Machi mwaka 2025.