Dk Abbas atoa maana ya “kuikosoa Serikali”

Msemaji Mkuu wa serikali Dk Hassan Abbas amekanusha uvumi unaonezwa na baadhi ya watu kuwa “kuikosoa Serikali ni marufuku”wakati alipokuwa anazungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam (TUDARCO). Picha| Rodgers Raphael.
- Amesema changamoto iliyopo ni kushindwa kutofautisha kati ya kuikosoa na kuitukana Serikali kwani wengi wamekuwa wakitukana na kusema wanaikosoa.
- Uhuru wa kutoa maoni umeelezwa vizuri katika Sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016 ambayo imekuwa ikilalamikiwa na baadhi ya wadau kuwa inaminya uhuru wa kujieleza.
Dar es Salaam. Msemaji Mkuu wa serikali Dk Hassan Abbas amewapinga vikali watu wanaosema “kuikosoa Serikali ni marufuku” kwasababu uhuru wa kutoa maoni umeelezwa vizuri katika Sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016.
Dk Abbas ametoa msimamo huo wakati akizungumza na wahadhili na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam (TUDARCO) kuhusu utekelezaji wa sheria hiyo nchini ambapo amesema mtu yeyote anaweza “kuikosoa Serikali”.
“Watu wanasema uhuru hamna kwa sababu haiwezekani kuikosoa serikali, huo ni uzushi unaweza kuikosoa serikali,” amesema Dk Abbas.
Pamoja na kutoa ufafanuzi huo, Dk Abbas amesema wadau wa vyombo vya habari nchini wanapaswa kutofautisha kati ya kuikosoa na kuitukana Serikali kwani wengi wamekuwa wakitukana na kusema wanaikosoa.
Amesema Wanahabari wanapaswa kufahamu haki zao za msingi wakati akitimiza majukumu ya kikazi ikiwemo kukusanya, kuhariri na kuchapisha habari ili kutekeleza haki ya watu wengine ya kupata taarifa sahihi.
Zinazohusiana:
- Wanahabari wahimizwa kuripoti habari za nishati jadidifu
- Wanahabari wahimizwa kuandika habari za kilimo, sayansi kukuza uchumi wa viwanda.
Akizungumzia utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, amewatoa hofu Wanahabari kwa kusema sheria hiyo itawezesha kuanzishwa Bodi ya urasimishaji wa wanahabari (Journalist accreditation Board) pamoja na Kamati ya malalamiko (complains committee) ambayo itasaidia kupunguza adha na kero za Wanahabari.
”Vyombo hivi vitakuwa mwamvuli kwa wadau wa sekta ya habari na waandishi wa habari kupeleka malalamiko yao,” amesema Dk Hassan
Katika maelezo yake amesema sheria hiyo imeweka wazi kwa mara ya kwanza tangu nchi kupokea uhuru mambo mbalimbali yenye manufaa kwa Wanahabari ikiwemo kutokuwahusisha wachapishaji endapo gazeti lolote litachapisha taarifa zisizo za ukweli.
Mwanafunzi wa chuo TUDARCO, Leyla Siraj amesema ufafanuzi wa utekelezaji wa sheria hiyo umemfungua macho kutokana na kuelewa maudhui yaliyopo ndani.
“Watu walikua wakilalamika sana juu ya sheria mpya lakini kumbe wengi hulalamika kwa maneno ya kuambiwa na wenzao ambao huenda hata hawajaisoma sheria hiyo, pia niimefahamu uzuri wa sheria hii kwa upana Zaidi,” amesema Siraj.
Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 alianza kutumika baada ya Rais John Magufuli kuweka saini Novemba 16, 2016 ikiwa ni siku chache ilipopitishwa na Bunge siku ya Novemba 5, 2016 Jijini Dodoma.
Licha ya mambo mazuri yanayotajwa katika sheria hiyo, bado utekelezaji wake na sheria kama Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015, Sheria ya Upatikanaji wa Habari ya mwaka 2016 ambazo zote zimekuwa zikilalamikiwa kwa kuminya uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kutoa maoni.