Wanahabari wahimizwa kuandika habari za kilimo, sayansi kukuza uchumi wa viwanda

August 28, 2018 12:31 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link
  • Wahimizwa kuandika zaidi habari za sayansi na kilimo kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda.
  • COSTECH, OFAB kuimarisha ushirikiano na vyombo vya habari.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo akiwa na Wanahabari waliowakilisha vyombo vyao katika upokeaji wa tuzo za umahiri wa habari za sayansi katika sekta ya kilimo. Picha| COSTECH.

Dar es Salaam. Waandishi wa Habari nchini wameshauriwa kubobea katika uandishi wa masuala ili kuongeza umahiri wa kuripoti habari zenye maslahi kwa jamii.   

Akizungumza katika utoaji wa tuzo za umahiri wa habari za sayansi katika sekta ya kilimo zilizofanyika jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo amesema kama Wanahabari watabobea katika fani zao itasaidia wananchi kupata taarifa sahihi na kuwawezesha kufanya maamuzi ya maendeleo.  

“Waandishi wabobee katika fani zao za uandishi, haiwezekani mtu mmoja, uandike kilimo, afya na michezo,” amesema Dk Akwilapo.

Wanahabari pia wametakiwa kuzifanyia tafiti habari wanazoandika na kutumia lugha nyepesi inayoendana na uelewa wa wananchi hasa waliopo vijijini.

Naibu katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Jim Yonazi amesema idadi ya Wanahabari wanaoripoti habari za sayansi bado ni ndogo jambo linalowanyima wananchi taarifa muhimu katika sekta hiyo.

“Kule kijijini watu hawaelewi mambo ya kisayansi, tutumie lugha nyepesi na rahisi waelewe  tafiti,” amesema Dk Yonazi na kuwataka Wanahabari wengi zaidi kuwekeza muda wao katika sekta hiyo.                              

Waandishi waliopata tuzo wametoa wito kwa waandishi wengine kuandika habari za kilimo ili kuwasaidia wakulima wanaotegemea sekta hiyo kutoa mchango katika ukuaji wa uchumi wa viwanda.

“Waandishi, tuandike vitu vitakavyotafutiwa ufumbuzi, mfano mimi nilivyoona wadudu wavamizi, nikaona niongee kwa kuandika” amesema Mwanahabari Fatma Abdul kutoka TSN aliyeshinda tuzo ya Mwandishi bora wa makala ya kilimo ambapo kazi yake itashindanishwa na Wanahabari wengine wa Afrika. 

Mshindi wa tuzo ya makala za redioni kutoka Uhuru FM, Helen Kwavava amesema Wanahabari wakitumia vizuri nafasi yao kuelemisha wakulima kuhusu matumizi ya teknolojia ya uhandisi jeni inayotumika kuzalisha mbegu zilizoboreshwa za GMO itawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kujipatia soko la uhakika. 

Kwa upande wake, Dk Beatrice Lyimo kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) amesema kuwa Wanahabri wanaoandika habari za sayansi ni wachache na lengo la kuandaa tuzo hizo ni kuhakikisha wanawajengea uwezo wa kuandika habari nyingi za sayansi na tafiti zake ili kuleta matokeo chanya katika sekta ya kilimo.

“Kwenye mashindano tuangalia zaidi usahihi wa habari za utafiti wa kisayansi ili waandishi wasipotoshe maana na tunataka waandishi waone urahisi wa habari za kisayansi ili watu waweze kuelewa,” amesema Dk Lyimo.

Utoaji wa tuzo kwa Wanahabari mahiri (Excellence in Science Journalism Award) umefanyika ikiwa ni hatua ya kutambua mchango wa vyombo vya habari vya Clouds Media, IPP Media, Sahara Group, SUA Media, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tanzania Standard Nation (TSN) na magazeti ya Uhuru na Mwananchi katika kuripoti habari za kilimo.

Waandishi waliopata tuzo za umahiri wa habari za sayansi kwenye kilimo ni Calvin Gwabara kutoka SUA Media, Fatma Abdul na Lucy Ngowi (TSN), Helen Kwavava (Uhuru FM) , Sifuni Mshana (IPP Media), Benson Eustace (Clouds Media), na Daniel Sembeye wa Business Times.

Enable Notifications OK No thanks