Deni la Serikali Tanzania laongezeka, lavuka Sh60 trilioni

June 10, 2021 8:26 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ndani ya mwaka mmoja deni hilo limeongezeka kwa zaidi ya Sh5 trilioni.
  • Serikali yasema bado deni hilo ni himilivu.

Dar es Salaam. Deni la Serikali nchini Tanzania limeongezeka hadi kufikia Sh60.9 trilioni Aprili 2021 kutoka Sh55.43 trilioni kipindi kama hicho mwaka jana kutokana kupokelewa kwa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Maendeleo.

Ongezeko hilo ni sawa na Sh5.47 trilioni ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba ameliambia Bunge leo Juni 10, 2021 kuwa kati ya deni hilo la Serikali, Sh43.7 trilioni au zaidi ya theluthi mbili za deni lote ni deni la nje huku deni la ndani likiwa ni Sh17.3 trilioni.

Katika hotuba ya Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 mwaka jana aliyekuwa Waziri wa Fedha Dk Isdory Mpango alisema hadi Aprili 2020, deni la Serikali lilikuwa Sh55.43 trilioni. Kati ya kiasi hicho, deni la nje lilikuwa Sh40.57 na deni la ndani Sh14.85 trilioni.

“Taarifa ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Desemba 2020 inaonyesha deni la Serikali ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu kwa kuzingatia ukomo wa viashiria vyote vinavyokubalika kimataifa,” amesema Dk Nchemba wakati akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22. 

Enable Notifications OK No thanks