DCEA yakamata kilo 3,182 za dawa za kulevya Tanzania
- Ni kutoka wilaya za Kigamboni, Ubungo, Kinondoni na wilaya ya Iringa.
- Dawa hizo zingeweza kuathiri watu milioni 76.3 ndani ya siku moja.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Tanzania (DCEA) imekatamata kilogram 3,182 za dawa za kulevya aina ya methamphetamine na heroini zilizoingizwa nchini kwa njia zizizo halali ambazo zingeathiri mamilioni ya watu nchini Tanzania ikiwemo nguvu kazi ya Taifa.
Kati ya hizo, kilogramu 2,180.2 ni methamphetamine na kilogramu 1,001.7 ni heroine zilizokamatwa katika Wilaya za Kigamboni, Ubungo, na Kinondoni jijini Dar es Salaam na wilaya ya Iringa mkoani Iringa katika oparesheni iliyofanyika kati ya Disemba 5 hadi25 mwaka huu huku watuhumiwa saba wakihusishwa na kosa hilo.
Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo, aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Disemba 27, 2023 jijini Dar es Salaam amesema kuwa hii ni mara ya kwaza kwa mamlaka hiyo kukamata kiasi hicho cha dawa za kulevya ambacho kingeharibu maisha ya vijana nchini.
“Hizi dawa tulizokamata walikuwa wameziweka kwenye vifungashio vya majani ya kahawa au majani ya chai, mbinu hii inatumika kurahisisha usafirishaji na kukwepa kubainika…
…Tumefanya oparesheni na kufanikiwa kukakamata kiasi hicho cha dawa za kulevya ambacho hakijawahi kutokea na halijawahi kukamatwa katika historia ya Tanzania,” amesema Lyimo.

Methamphetamine na heroine zinaweza kutumiwa ikiwa katika mfumo wa unga, sindano au vidonge.Picha|Faith Recovery Centre
Kwa mujibu wa Lyimo dawa hizo zilizokamatwa zinauwezo wa kuathiri watu milioni 76.3 ndani ya siku moja na kusababisha hatari katika mfumo wa fahamu.
Kiasi hicho cha dawa zilizokamatwa zingeweza kuathiri zaidi ya watu milioni 61 waishio Tanzania na wengine kutoka nchi jirani na kusababisha madhara ya kudumu kwenye ubongo na hivyo kupunguza uwezo wa kutunza kumbukumbu na kuathiri mfumo mzima wa fahamu.
Kwa mujiu wa Lyimo madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya aina ya methamphetamine hayana matibabu jambo linaloweza kusababisha kifo au ulemavu wa kudumu.
Soma zaidi:Mila, desturi zilizopitwa wakati, sababu ongezeko la VVU Mwanza
Msako wa wauzaji wa dawa za kulevya kuendelea
Aidha, Lyimo amesema bado DCEA itaendeleza msako wa wauzaji wa madawa ya kulevya waliojificha au kutorokea nchi jirani ili kuhakikisha biashara ya madawa ya kulevya inamalizika nchini.
“Hakuna atakayepona katika oparesheni hii…mamlaka imeamua na imejidhatiti kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wote wa dawa za kulevya tutawasaka, tutawakamata na kuhakikisha biashara ya dawa kulevya si rafiki kwao…Natoa onyo kwa wote wanaoendelea kujishughulisha na dawa za kulevya hapa nchini kuacha na wajikite kwenye biashara nyingine halali,” ameeleza Lyimo.
Lyimo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa DCEA kwa kuwafichua wauzaji wa madawa ya kulevya pamoja na mtandao mzima unaofanya biashara hiyo haramu kwa kutumia simu ya bure ya 119 na kutoa taarifa za wahalifu hao ambazo zinawasaidia kufanya oparesheni na kuwatia nguvuni watuhumiwa wote.
Latest