CRDB, Funguo, waunganisha nguvu kuongeza ufadhili kwa ‘startups’, MSMEs Tanzania 

September 10, 2024 5:51 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Kutokana na ushirikiano huo waombaji kunufaika na ufadhili pamoja na mikopo nafuu.
  • Maombi kutumwa kupitia njia ya mtandao.

Dar es Salaam. Huenda wamiliki wa biashara ndogo na za kati (MSMEs) sambamba na kampuni chipukizi nchini (startup) wakapata ahueni ya upatikani wa mitaji baada ya uzinduzi wa ushirikiano wa pamoja kati ya programu za Funguo Innovation na iMBEJU katika kupanua wigo wa upatikanaji wa fedha za mitaji kwa kampuni hizo.

Ushirikiano huu unalenga kuchanganya ruzuku zisizorudishwa ‘grant’ kutoka Programu ya Funguo na mikopo nafuu inayorudishwa kutoka Imbeju, ili kuongeza nafasi kwa wafanyabiashara wenye kampuni ndogo kupata mikopo.

Imbeju ni mpango wa taasisi ya benki ya CRDB inayotoa ufadhili endelevu kwa wajasiriamali kupitia mikopo nafuu ikiunga mkono mawazo ya biashara yanayoweza kupanuka na kuifaidisha jamii kwa kiasi kikubwa, pia unatoa zana muhimu kwa vijana, wanawake na makundi maalum kama elimu ya kifedha, ujuzi wa ujasiriamali na mafunzo ya usimamizi wa biashara.

Aidha, Mpango Bunifu wa Funguo ‘The Funguo Innovative Programme’ ni mpango ulioanzishwa ili kuchochea ubunifu na kusaidia kuanzisha biashara mpya na biashara ndogo na za kati (MSMEs) nchini Tanzania, ukilenga kuongeza idadi ya kampuni bunifu zinazofanikiwa kwa kuchangia katika malengo ya maendeleo ya kitaifa na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ukifadhiliwa na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa ‘UNDP’.

Joseph Manirakiza, Meneja wa Programu wa Funguo Innovation, UNDP Tanzania amebainisha wameungana na Benki ya CRDB kuunganisha nguvu ili kuwakikia vijana wengi wanaopambana kujitengenezea ajira ambapo hadi sasa Funguo imetoa ufadhili wa Sh3.8 bilioni kwa kampuni arobaini na tatu (43) nchini.

Kwa mujibu wa Manirakiza waombaji wanaweza kupata fedha kupitia ruzuku za kichocheo ‘catalystic grants’ za Funguo ambazo huwa kati ya Sh50 milioni hadi Sh100 milioni au mikopo nafuu ya iMBEJU kuanzia Sh30 milioni au zaidi kulingana na uwezo wa biashara na uwezo wa kulipa.

Tully Mwambapa, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya CRDB Foundation, aliyekuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ushirikiano huo amesema kupitia programu ya Imbeju benki hiyo imetoa ufadhili wa zaidi ya Sh400 milioni kwa kampuni nane (8) chipukizi. 

“Tuna furaha kushirikiana na Funguo kwa sababu tunaamini sasa tutaweza kufikia idadi kubwa ya kampuni changa na kuwawezesha kukua na kuleta kampuni changa zaidi,” amesema Mwapamba.

Vigezo vya kampuni kustahili ufadhili 

Ili kupata ufadhili wa mkopo wa mtaji Funguo na Imbeju wameainisha vigezo vya msingi ambavyo kampuni inatakiwa kuwa navyo kabla ya kuwasilisha maombi yao ili kuongeza nafasi zao za kufanikiwa kupata ufadhili unaotolewa.

Awali kampuni inatakiwa iwe na hadhi ya kutambulika kama chipukizi ‘startup’ na iwe  inafanya biashara zinazo tengeneza faida au kampuni za kijamii zinazolenga masoko.

Balozi wa Umoja wa Ulaya Tanzania Bi Christine Grau akieleza utayari wao kutoa ufadhili kwa kampuni chipukizi. Picha |EU in Tanzania

Inatakiwa kuwa imesajiliwa kisheria nchini Tanzania pamoja na kumilikiwa kwa asilimia 51 au zaidi na raia wa Tanzania.

Vigezo vingine ni kuwa imevuka hatua za awali za uanzilishi ambazo ni wazo ‘ideation’ na majaribio ‘pilot stage’ ikiwa na bidhaa ambazo tayari zinavutia walaji na watumiaji na kukubalika sokoni.  

Aidha, kampuni inapaswa kuwa haijafikisha ufadhili wa zaidi ya milioni 273 au Dola 100,000 za Marekani kupitia hisa au mkopo muda wa uombaji.

Jinsi ya kufanya maombi

Muombaji anaekidhi vigezo na kuhitaji ufadhili wa programu hii anapaswa kujaza fomu ya maombi kamili inayopatikana mtandaoni kwenye kiungo hichi https://funguo.org/call-for-funding-2/ kilichopo kwenye tovuti ya ‘The Funguo Innovation Programme’, na kujaza kwa usahihi.

Mtumaji anapaswa kuzingatia kuwa lazima maombi yake yawasilishwe kupitia mtandao pekee, maombi yatakayowasilishwa kupitia njia hii yakiwa na nyaraka zote muhimu tu ndiyo yatakayozingatiwa.

Nyaraka hizo zinajumuisha dondoo za mpango wa biashara zinazotumika kuwasilisha wazo la biashara, huduma, au bidhaa kwa wawekezaji au wadau wengine, kwa lengo la kupata ufadhili au msaada mwingine wa kibiashara.

Nyaraka nyingine ni za uthibitisho wa usajili wa kampuni, uthibitisho wa umiliki wa hisa, kama vile katiba na makubaliano ya kampuni, makadirio ya kifedha ya miaka miwili, wasifu wa wafanyakazi na nyinginezo.

Mfumo huo wa maombi mtandaoni unamruhusu muombaji kuanza mchakato wake kisha     kuhifadhi atakapoishia na kurudi kukamilisha baadaye.

Balozi wa Umoja wa Ulaya Tanzania ambao ni miongoni mwa wafadhili wa Programu hiyo Christine Grau amesema 2023 kampuni changa zilipata Sh67.8 bilioni kutoka kwa wafadhili wa kigeni, kiasi ambacho ni kidogo sana ikilinganishwa na nchi nyingine, lakini kwa upande mwingine, kampuni changa pia zilipata uwekezaji wa ndani wa Sh62.4 bilioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks