Corona ilivyochangia kuimarisha muziki wa taarab Zanzibar
- Umesaidia wanamuziki kujinoa na kupata muda mwingi kutunga nyimbo.
- Imefungua fursa ya matamasha ya mtandaoni.
- Serikali yaahidi kuukuza muziki huo wakati ikipambana na Uviko-19.
Zanzibar. Katika Chuo cha Muziki wa Asili Zanzibar (DCMA) kilichopo eneo la Stone Town, nakutana na mwanadada aliyevalia ushungi mweusi na nilipoulizia nafikaje kwa wanamuziki, mwanadada huyo mwenye tabasamu ambalo siwezi kulisahau, aliniambia, “fuata muziki” huku kidole chake kikionyesha ngazi zilipo.
Nilipanda ghorofa ya kwanza kuelekea ya pili na nilikaribishwa na ukuta uliokuwa umepambwa na nota za muziki wa “Yalaiti” uliowahi kuimbwa na malkia wa muziki wa taarab, Bibi Kidude na baadaye kurudiwa na Mwana FA akishirikiana na Linah kwa maadhi ya Bongo Fleva na HipHop.
Katika ghorofa ya tatu ya jengo hilo, ndipo sauti za watu zilitokea huku katika varanda ya DCMA, kilikuwepo kikundi kilichoonekana kuwa katikati ya kutengeneza maudhui ya tangazo kwa ajili ya tamasha la muziki.
Ni bendi ya muziki wa asili ya Pwani ya “Siti and The Band”. Hapo walikuwa wakitengeneza video ya kuvutia mashabiki wa muziki wao.
Siti and the Band wanafanya muziki wa kizazi kipya na taarab ya kizazi kipya. Hadi sasa wameshirikiana na wasanii wengine akiwemo G Nako Wara wara katika kutengeneza muziki wa maadhi ya asili ya Kitanzania.
Wanakikundi wote walikuwa wamejaa tabasamu na walicheka kila mara mmoja wao alipokosea na kuwalazimu kurudia tangazo.
Kicheko hicho siyo bure bali kinaashiria jinsi walivyovuka salama na kuendelea na maisha ya muziki licha ya janga la ugonjwa wa Corona (Uviko-19) kuathiri utendaji wa tasnia ya muziki na burudani duniani.
Wanamuziki na wasanii mbalimbali waliathirika kimapato kutokana na kupungua kwa matamasha na utumbuizaji wa moja kwa moja katika kumbi mbalimbali.
Hata hivyo, kwa bendi inayojihusisha na muziki wa taarab asilia haikua changamoto kubwa kwa sababu walitumia njia mbadala kuushinda Uviko-19 na kuendelea na shughuli zao za muziki.
Siti Amina akiwa kwenye moja ya matamasha waliyowahi kufanya na bendi ya Siti. Picha| Lorenz Herrmann.
Walivyoishinda Corona
Janga la Uviko-19 limekuwa fursa kwa bendi hiyo iliyoasisiwa mwaka 2016 kujijenga na kutafuta njia endelevu za kuendelea kuwepo katika tasnia ya muziki kwa muda mrefu.
Tangu Uviko-19 uingie Tanzania Machi 2020, walitumia muda huo kutengeneza albamu ambayo wanatarajia kuiachia sokoni mwakani huku wakijitengenezea jina miongoni mwa wazawa kwa kushiriki shughuli za kijamii ikiwemo kutoa elimu ya ugonjwa huo na kuendelea kujifua kimuziki.
Meneja wa bendi hiyo, Lorenz Herrmann ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa baada matamasha kupigwa marufuku ilimlazimu kutafuta vyanzo vipya vya mapato ili kuendesha muziki na kulipa wafanyakazi mishahara.
“Tulipata ufadhili kutoka shirika la Hivos East Africa uliotusaidia kuendelea na kazi za muziki, kurekodi albamu na video,” anasema Herrmann na kuongeza kuwa waligeukia matamasha ya mtandaoni ili kutopoteza mashabiki wao.
“Pia tulipata ufadhili kutoka kwa “The Music In Africa Foundation” kufanya matamasha ya mtandaoni ambayo imelipa kidogo wasanii kwa kuwawezesha kujiendeleza kwa mwezi mmoja, miezi miwili,” anasema Herrmann.
Meneja huyo anasema kuvuka salama katika janga hilo kumechangiwa pia na ndoto kubwa ya muziki waliyonayo wanachama wa bendi hiyo na hivyo hakupenda kuona Corona ikizivunja.

Hali ilivyokuwa kabla ya Uviko-19
Kwa Zanzibar, ni vigumu kutaja bendi za muziki wa asili bila kuitaja bendi hiyo.
Kutokana na umaarufu wake ilikuwa ikipata mialiko mbalimbali yakiwemo matamasha ambayo yaliihakikishia mapato kwa ajili ya wanamuziki wake.
Uongozi wa bendi hiyo umeeleza kuwa walianza kulipa mishahara ya hadi Sh500,000 kwa mwezi kwa wanachama wake lakini baada ya Uviko-19 walitetereka katika eneo hilo lakini siyo kuanguka kabisa.
Hata hivyo, wanachama wawili wa bendi hiyo hawakuendelea na safari hiyo na wakaacha na kugeukia shughuli nyingine.
Kabla ya Uviko19, ilikuwa ni kawaida kwa wanakikundi hawa kuwa na uhakika wa kutumbuiza si chini ya mara mbili kila wiki huku wana kikundi mmoja mmoja kuwa na kazi nyingine nje ya bendi.
Walikuwa na mikataba ya kufanya kazi na taasisi mbalimbali ikiwemo hoteli ya Kendwa Rocks lakini Corona ilitwaa mafanikio yote hayo.
“Tulikuwa tayari tumeshika soko hata katika hafla za Serikali,” anasema Amina Omary Juma (Siti Manina), kiongozi, mwimbaji na mpiga oud (gitaa) katika bendi hiyo.
Changamoto hizo zote ndiyo ziliwafanya kuimarika na kujinoa zaidi ili kuendelea kuwepo katika soko la ushindani mpaka sasa, wakati ambao bendi nyingine zimefungasha virago.
Baadhi ya wanamuziki wa “Siti and The Band” wakifanya mazoezi hivi karibuni Zanzibar. Picha| “Siti and The Band”.
Matumaini yaliyotukuka
Licha ya kuwa hali bado haijarudi kama ilivyokuwa awali, wanachama wa bendi hiyo wanasema wanaoiona kesho yao ikiwa ang’avu kuliko jana.
Wana matumaini makubwa ya kuanza kutumbuiza katika matamasha na shughuli mbalimbali kutokana na hatua zilizochukuliwa kupambana na Uviko-19 ikiwemo utoaji chanjo na kulegezwa kwa masharti ya usafiri wa kimataifa.
Mkurugenzi wa muziki wa bendi hiyo, Sam Grove anaamini kuwa hali zao za kiuchumi zitaimarika tena kwa sababu watalii wameanza kuingia visiwani humo na hao ndiyo wateja wao wa uhakika.
“Kwa sasa hivi hatuna kazi “permanent” (za kudumu) za kusema kila wiki lakini siyo haba, ukikusanya hizo shoo mbili tatu walau kwa mwezi unaweza kupata hata Sh400,000 kwa kiasi cha chini,” anasema Grove.
Siyo tu kupata wageni lakini maono yao kwa sasa ni kupata safari za kimataifa ili kwenda kuitangaza Tanzania kwa muziki wa asili wa Taarab ili kukuza soko la shughuli zao.
Mpiga ngoma wa bendi hiyo, James Simon anayetegemea muziki kwa asilimia 80 kuendesha maisha yake anasema anafurahi kuona utoaji wa chanjo ya Uviko-19 umeanza kufungua fursa za kusafiri nje ya nchi na yeye yuko tayari kuchanja kuzipata fursa hizo.
Serikali yawashika mkono
Kwa kutambua athari za Uviko-19 kwa wasanii wa muziki, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeendelea kuwashika mkono pale inapoweza ikiwa ni njia za kuendelea kuutangaza muziki kimataifa na kitaifa pia.
Afisa Utalii Mkoa wa Mjini Magharibi, Said Soud Said anasema Serikali inawahusisha wanamuziki katika shughuli mbalimbali za utalii na kiserikali ili kuwapunguzia machungu ya Uviko-19 kwa kujipatia kipato.
“Kuna vikundi vya taarab asilia ambavyo vimetafutwa kwenye ziara ya “The Royal Tour” ya Mama Samia Suluhu Hassan na walitumbuiza wakati wa ziara hiyo,” anasema Said.
Anasema Serikali itaendelea kufanya juhudi mbalimbali kuirejesha hali ya utalii Zanzibar kama ilivyokuwa awali kwa kutengeneza matangazo na kutoa mafunzo ya kujikinga dhidi ya Corona kwa watu.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Latest