Chadema: Uchaguzi wetu utakuwa huru na wazi

January 7, 2025 4:25 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Chasema kitatoa nafasi kwa vyombo vya habari kushiriki mchakato huo, licha ya kwamba si wajumbe wa kikatiba.
  • Viongozi wa dini, taasisi za kimataifa kualikwa kuwa waangalizi.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema uchaguzi wa viongozi wa chama hicho kitaifa utakuwa huru na wa wazi ikiwa ni sehemu ya kusimamia misingi ya demokrasia inayohubiriwa na chama hicho.

Ahadi hiyo imetolewa leo Januari 7 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika aliyekuwa akizungumza na vyombo vya habari kwenye mkutano uliofanyika makao makuu ya chama hicho Mikocheni, Dar es Salaam.

Mnyika ameeleza kuwa, chama hicho kitatoa nafasi kwa vyombo vya habari kushiriki mchakato huo, licha ya kwamba si wajumbe wa kikatiba, ili kuhakikisha taarifa za uchaguzi zinafika kwa uwazi kwa wanachama na umma kwa ujumla.

“Ili kuhakikisha uwazi katika uchaguzi tutaweka mazingira katika ukumbi wa uchaguzi ambayo yataruhusu vyombo vya habari pamoja na kuwa sio wajumbe wa kikatiba, sasa ni vyombo vingapi kwa utaratibu upi hayo tutaendelea kushauriana kadri tunavyoendelea na mchakato wa maandalizi ya uchaguzi,” amesema Mnyika.

Kauli ya Mnyika inakuja muda mfupi mara baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara Tundu Lissu ambaye pia anagombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho kupendekeza kuwaalika viongozi wa dini na wa taasisi za kimataifa kuwa waangalizi wa uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Januari 21, 2025.

Hata hivyo, Mnyika ameeleza kuwa taasisi mbalimbali, ikiwemo zile za kimataifa na za kidini, zimealikwa kuwa watazamaji wa uchaguzi huo, hatua inayolenga kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa uhuru na haki bila kuacha mianya ya rushwa au hujuma zozote.

Wagombea 300 wapewa onyo

Katika hatua nyingine, Mnyika amewataka wagombea wa nafasi mbalimbali kuzingatia katiba, kanuni, maadili ya wanachama na viongozi sambamba na miongozo mbalimbali husasan ya taratibu za kuendesha kampeni za uchaguzi ndani ya chama (2012) pamoja na mwongozo wa chama dhidi ya rushwa wa 2012.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, mgombea atayekiuka kanuni cha uchaguzi atapewa adhabu kulingana na maamuzi ya kamati kuu ya Chadema.

“Mgombea yeyoye ataekiuka taratibu na kanuni hizi atachukuliwa adhabu zifuatazo, moja ni kupewa onyo. Pili, kupewa onyo kali. Tatu, kuondolewa kwenye mchakato wa uchaguzi…

…Nne, kufungiwa kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama kwa muda utakao amriwa na mamlaka husika, isipokuwa muda hautazidi miaka mitano,” amesema mnyika.

Sambamba na hilo amebainisha kuwa wagombea wenye malalamiko au hawaridhiki na jinsi mchakato wa uchaguzi unavyoendelea watoe mapendekezo yao rasmi kupitia maandishi. 

“Mgombea mwenye mapendekezo ambayo hayamo kwenye kanuni za Chama ambayo yanatekelezeka, aandike barua rasmi ya mapendekezo yake,” amesema Mnyika.

Uchaguzi wa Chadema unaotarajiwa kufanyika Januari 21, unahusisha jumla ya wagombea 300 watakaochuana kugombea jumla ya nafasi 23, zikiwepo nafasi mbili za juu zinaoonekana kuwa na ushindani mkali kati ya viongozi wa ngazi ya juu wa chama.

Nafasi hizo ni ya Mwenyekiti wa chama bara inayowaniwa na wagombea watatu, Tundu Lissu, Freeman Mbowe, na Odero Odero. Sambamba na ya Makamu Mwenyekiti Bara inayowaniwa na wagombea watatu pia ambao ni, John Heche, Ezekia Wenje na Mathayo Geko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks