CCM yabadili ratiba uchukuaji fomu ubunge, udiwani, uwakilishi
- Ni baada ya mashauriano na wanachama wake, kutafakari na kupima kwa umakini shauri hilo.
- Zoezi litaanza rasmi Juni 28, 2025 na kukamilika Julai 2, 2025 kwa kufuata utaratibu ule ule uliotangazwa awali.
Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza marekebisho ya ratiba ya mchakato wa ndani wa uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo sasa zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa ajili ya ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na udiwani litaanza rasmi Juni 28, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili 15, 2025 na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, mabadiliko hayo yamefanyika kufuatia mashauriano na wanachama wake pamoja na kutafakari kwa kina ushauri uliotolewa.
“Baada ya mashauriano na wanachama wake, kutafakari na kupima kwa umakini ushauri huo, kimeamua kufanya marekebisho juu ya ratiba ya mchakato wa ndani wa uteuzi wa wagombea kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa mchakato utaanza Juni 28, 2025 saa 2:00 asubuhi na kukamilika Julai 2, 2025 saa 10:00 jioni, kwa kufuata utaratibu ule ule uliotangazwa awali kupitia taarifa ya Aprili 10, 2025.
Awali CCM ilipanga kuanza zoezi hilo Mei 1 hadi Mei 15, 2025 ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, wanachama wa CCM wanaotaka kugombea nafasi ya ubunge au ujumbe wa Baraza la Wawakilishi watatakiwa kuchukua na kurejesha fomu kwa Katibu wa CCM wa Wilaya husika.
Kwa upande wa wanachama wanaotaka kugombea Viti Maalumu kupitia makundi mbalimbali kama UWT, UVCCM, Wazazi, pamoja na makundi ya NGOs, wafanyakazi, wasomi na watu wenye ulemavu, watatakiwa kuchukua na kurejesha fomu kwa makatibu wa jumuiya hizo katika mikoa husika.
Aidha, wagombea wa nafasi ya udiwani watachukua na kurejesha fomu kwa makatibu wa kata au wadi zinazohusika, kulingana na eneo walilokusudia kugombea.
CCM imesisitiza kuwa pamoja na mabadiliko haya ya tarehe, utaratibu wa kuchukua na kurejesha fomu unabaki kama ulivyopangwa awali, na kuwataka wanachama wote kufuata maelekezo kwa wakati.
Kwa mujibu wa Dk Nchimbi, lengo la marekebisho hayo ni kuhakikisha mchakato wa ndani unatekelezwa kwa umakini na kwa kuzingatia ushauri uliotolewa na wadau mbalimbali ndani ya chama.
Latest



