CCM: Tamisemi puuzieni makosa madogo tufanye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024

November 12, 2024 6:28 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kukosea herufi za majina,tarehe na miaka ya kuzaliwa. 
  • Wadau wa siasa wataka michakato ya uchaguzi iwe huru na haki na kutotegemea utashi wa kisiasa.

Arusha. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeiomba Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kupuuzia baadhi ya makosa yaliyofanywa na wagombea wakati wa kujaza fomu ili uchaguzi uwe na wagombea wengi kwa kuwa demokrasia ya Tanzania bado changa.

Tamisemi kupitia halmashauri ndio wanasimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 ambapo nafasi zinazowaniwa ni pamoja na uenyekiti wa kijiji, kitongoji pamoja na wajumbe wa Serikali za Mitaa.

Kwa siku za hivi karibuni baadhi ya vyama vya siasa vimekuwa vikitoa matamko ya kutoridhishwa na jinsi mchakato wa kuchukua fomu pamoja na kupitisha wagombea ulivyoendeshwa wakibainisha maelfu ya wagombea wao kukatwa majina.

Hata hivyo, Waziri wa Tamisemi Mohamed Mchengerwa alivitaka vyama vya siasa  kuwaelekeza wagombea ambao hawakuridhika na mchakato huo kuweka mapingamizi kama ambavyo sheria ya uchaguzi huo inataka.

CCM kupitia kwa Katibu Mkuu wake Dk Emmanuel Nchimbi aliyekuwa akizungumza na wanahabari amesema ombi la chama chake limetokana na mazungumzo kati yake na Mwenyekiti wa CCM Samia Suluhu Hassan ambapo pamoja na mambo mengine wamebaini demokrasia ya Tanzania bado ni changa na bado kuna mambo mengi ya kujifunza kuhusu uchaguzi huo.

“Tunatambua kuwa watendaji wa ngazi ya halmashauri wanafata sheria lakini ni uhimu kujua kuwa demokrasia yetu bado ni changa inahitaji muda wa kukua lakini watu wetu hawajazoea sana vitu hivi,” amesema Dk Nchimbi jijini Dar es Salaam leo Novemba 12, 2024.

Miongoni mwa makosa aliyotaja Dk Nchimbi yanayotakiwa kupuuziwa ni pamoja na kukosea herufi za majina, kukosea tarehe na miaka ya kuzaliwa. 

Kwa mujibu wake makosa hayo yanaweza kurekebishika hivyo kutoa nafasi kwa watu wengi zaidi kugombea katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.

Mbali na makosa hayo, Dk Nchimbi ameyataja makosa mengine yasiyotakiwa kupuuziwa ikiwemo yale yanayokinzana na Katiba ya Tanzania na sheria za uchaguzi huo ikiwemo wanaume kugombea katika nafasi za viti maalum ambazo ni kwa ajili ya wanawake.

Hata hivyo, bado uamuzi huo wa CCM haujapokelewa vyema na wadau wa kisiasa ambao wamesisitiza michakato ya uchaguzi kuwa ya huru na haki kwa pande zote na kutotegemea utashi wa kisiasa wa kiongozi au chama kilichoko madarakani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks