Bustani za matumbawe na uzuri uliojificha Ghuba ya Tanzania

February 10, 2020 7:58 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni hifadhi ya bahari yenye ukubwa zaidi ya kilometa za mraba 600 inayopatikana kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
  • Urefu wa kilometa 45 unaifanya kuwa sehemu mahususi kwa wapiga mbizi watakaofurahia kuwaona nyangumi, pomboo na bustani za matumbawe.
  • Kwenye hifadhi hii, unaweza kupiga picha na video.

Dar es Salaam. Hata baada ya kuzitembelea mbuga za wanyama na hifadhi za Taifa zote za Tanzania, hauna haja ya kushika kichwa kwa kujisifu umekamilisha shughuli ya utalii.

Zaidi unahitaji kuweka viatu na miwani yako kando na kuanza kununua vifaa kwa ajili ya utalii wa baharini.

Umejiandaa? Ambatana na Nukta Safari katika mwendo huu wa kukufungulia milango ya fukwe za bahari zitakazokuacha mdomo wazi huku uso wako ukijaa mshangao kwa kutozifahamu sehemu hizo.

Leo tunaanza safari hii na hifadhi ya bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingiliano ya Mto Ruvuma. Je, umewahi kuisikia? Kama bado, haya ndiyo unatakiwa kuyafahamu.

Hifadhi hii ambayo ni ya pili kwa ukubwa ikiwa ni kwa mujibu wa Taasisi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu ya nchini Tanzania, ukubwa wake unafikia kilometa za mraba 650.

Ghuba hiyo inayopatikana kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara ni hifadhi mahususi kwa kuogelea kwani kati ya kilometa hizo, kilometa 430 ni za bahari.

Kwa kuitembelea hifadhi hii utapata nafasi ya kuogelea katika pwani yenye urefu wa kilometa 45 inayowafaa wadau wa kupiga mbizi huku ukipata nafasi ya kutembelea visiwa vitatu vya Namponda, Membelwa na Kisiwa Kidogo.

Kwa kuitembelea hifadhi hii utapata nafasi ya kuwaona pomboo na wanyama bahari wengine wakiwemo nyangumi. Picha| TIF.

Kwanini utembelee hifadhi hii ya Ghuba?

Mbali na changamoto za uvuvi haramu ambazo zinatesa fukwe na hifadhi nyingi za bahari nchini Tanzania, hifadhi hii bado imebaki kuwa na bustani za matumbawe na makazi pendwa ya nyangumi, pomboo na kasa.

Utafurahia hifadhi hii baada ya kupiga mbizi na kuziona nyasi za baharini huku ukifurahia harufu nzuri itokanayo na majani ya misitu ya mikoko.

Kama kuogelea siyo fungu lako, bado una nafasi ya kuweka kambi za usiku, kutembea na kulala kwenye mchanga safi ama kuvinjari kwa boti.

Mfuko wako utune kwa kiasi gani?

Kwa mujibu wa Taasisi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu ya nchini Tanzania, hauwezi kuyaona haya yote bila hata kulichangia Taifa. 

Kama wewe ni mgeni umevuka umri wa miaka 15, utahitaji Sh54,523 na kama upo chini ya hapo utachangia Sh27,261.

Endapo unaambatana na mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano, ataona uzuri huo bila tozo yoyote huku akijiandaa kurudi pale atakapokuwa mkubwa kuufaidi zaidi.

Kwa Watanzania, mtoto chini ya miaka mitano ataingia bure huku mwenye miaka mitano hadi 15 atachangia Sh1,180. Kwa mwenye umri zaidi ya miaka 15, Sh2,360 itakuwa ni mchango tosha.


Zinzohusiana


Endapo utataka kuweka kambi, Sh54,280 itakuhusu huku Sh2.7 milioni ikikuhusu endapo utahitaji kupiga picha za mnato na video kwa siku saba ikiwa ni kwa ajili ya biashara. 

Hakika hautojutia kuona sehemu ya uzuri huu wa Tanzania ambao unafikika kwa usafiri wa magari ya abiria na pia ya kukodi ambayo yatakutembeza kwa umbali wa kilometa 50 kutoka pwani ya Msimbatu iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.

Enable Notifications OK No thanks