Ifahamu miezi mitukufu kwa Waisilamu na umuhimu wake

February 7, 2025 2:05 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Miongoni mwa miezi hiyo ni Dhul-Qaada, Dhul-Hijjah na Rajabu.

Dar es Salaam. Kwa waumini wa dini ya Kiislamu, miezi mitukufu si sehemu ya mfumo wa kawaida wa kalenda ya kimuundo, bali ni miezi yenye umuhimu wa kiimani kulingana na mafunzo ya Qur’ani Tukufu. 

Ndani ya mafunzo hayo Mwenyezi Mungu ameeleza kuwa miezi ya Kiislamu ni kumi na mbili, lakini miongoni mwa hiyo, minne ni mitukufu.

Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, miezi hii minne haijafanywa mitukufu kwa bahati mbaya bali ni miezi ya amani, ibada maalum na matukio makubwa ya kihistoria yanayohusiana na imani ya Kiislamu. 

Kulingana na Sheikh Salim Qahtwan, kiongozi na mwalimu wa dini ya Kiislamu kutoka mkoani Tanga, miezi mitukufu ni Dhul-Qaada, Dhul-Hijjah, Muharram, na Rajab.

Dhul-Qaada

Mwezi wa Dhul-Qaada ni wa kumi na moja katika kalenda ya Kiislamu. 

Umekuwa mtukufu kwa sababu katika kipindi cha zamani, watu walihitaji usalama wa kutosha ili kuanza safari za Hajj kulingana na vita vilivyokuwa vikiendelea wakati wa zama hizi.

Mwezi huu umeteuliwa kuwa mtukufu ili kuweka mazingira ya amani, hasa kwa wale wanaojiandaa kwenda kutekeleza ibada ya Hajj.

Dhul-Hijjah

Mwezi wa Dhul-Hijjah ni wa kumi na mbili katika kalenda ya Kiislamu, na ni kipindi muhimu kwa Waislamu. 

Katika mwezi huu, ibada ya Hajj, ambayo ni moja ya nguzo tano za Uislamu, hufanyika. 

Aidha, mwezi huu unahusisha sikukuu ya Eid al-Adha, ambapo Waislamu hutekeleza ibada ya kuchinja wanyama kama alama ya kujitolea kwa Mwenyezi Mungu.

Sikukuu hii hufanyika siku ya kumi ya Dhul-Hijjah.

Muharram

Mwezi wa Muharram ni wa kwanza katika kalenda ya Kiislamu na umebeba historia muhimu kwa Waislamu. 

Sheikh Qahtwan anasema mwezi huu unaadhimishwa kwa kumbukumbu ya anguko la Firauni (jina walilokuwa wakiiitwa wafalme wa zamani wa Misri).

“Ndio siku ambayo watu wanasherekea siku aliyoangamia dhalimu mkubwa duniani aliyekuwa akichinja watoto, anadhurumu watu,” amesema sheikh Qahtwan. 

Umetajwa kuwa mtukufu kwa sababu pia unatoa fursa ya amani kwa wale waliotoka Hajj kufanya ibada kurejea salama.

Mufti wa Kipalestina wa Hebron anatumia darubini ya kielektroniki kuangalia mwezi mwandamo unaotangaza mwanzo wa mwezi wa Ramadhani. Picha /Middle East Eye.

Rajab

Rajab ni mwezi wa saba katika kalenda ya Kiislamu na ni moja ya miezi mitukufu. 

Tukio muhimu linalohusiana na mwezi huu ni Isra’ na Mi’raj, safari ya usiku ya Mtume Muhammad (SAW) kutoka Makka hadi Yerusalemu na kupaa kwake mbinguni.

Sheikh Qahtwan amebainisha kuwa mwezi huu uliteuliwa kuwa mtukufu ili kuruhusu waumini kutoka sehemu mbalimbali kufanya Umrah kwa amani na kutembelea Al-Ka’bah bila vikwazo.

Je, vipi kuhusu Ramadhani?

Kwa mujibu wa Sheikh Qahtwan, Ramadhani si miongoni mwa miezi mitukufu, lakini ni mwezi uliobora zaidi kutokana na fadhila zake, ikiwa ni pamoja na swaumu na matendo mema yanayopendekezwa.

“ katika lugha ya kiswahili tunapata shida wakati mwingine kutohoa maneno, tukisema utukufuu Ramadhani pia tunaita mtukufuu kulingana na fadhila zake, angalau kutofautisha tutafute msamiati mwingine,” amebainisha sheikh Qahtwan.

Sheikh Hashim Rusaganya naye ameongeza kuwa, ndani ya Qur’ani Tukufu (sura ya Tawbah, aya ya 36), Mwenyezi Mungu ametaja wazi miezi minne mitukufu. 

Miezi hii ni sehemu ya nidhamu ya kiimani na mafunzo kwa Waislamu kudumisha amani na ucha Mungu.

Kwa ujumla, miezi mitukufu kwa Waislamu ni alama ya utukufu wa kiimani na wakati wa kujitathmini, kufanikisha ibada muhimu, na kuendeleza amani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks