Serikali yawataka wafanyabiashara Kariakoo kusitisha mgomo ikiahidi kutatua kero zao

May 15, 2023 2:40 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya Waziri Mkuu kuzungumza na wafanyabiashara hao.
  • Atoa maagizo ya kusitisha vikosi vya ukusanyaji kodi na kusimamisha sheria za kodi zilizoanza kutekelezwa.
  • Wafanyabiashara wakubali ombi la Serikali huku Naibu Spika akiahidi kushughulikia waliodharau kauli ya Rais bungeni.

Dar es Salaam. Serikali imewataka wafanyabiashara wa Soko la kimataifa la Kariakoo na kufungua maduka kuendelea na shughuli zao huku ikiahidi kuzifanyia kazi changamoto zote za kikodi walizoibua katika mgomo wao. 

Kauli hiyo ya Serikali inakuja mara baada ya mgomo wa zaidi ya saa 12 uliofanywa na wafanyabiashara wa soko la Kariakoo ambao walikuwa wakilalamikia ukusanyaji mbovu wa kodi, kuanzishwa kwa kodi ya ghala pamoja na kamata kamata inayofanywa na vikosi kazi (task forces).

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekuwa akizungumza na wafanyabiashara haokatika soko la Kariakoo leo Jumatatu Mei 15, 2023 amewaambia kuwa Serikali imepokea kero zao zote na inakwenda kuzifanyia kazi lakini kutokana na umuhimu wa Soko la Kariakoo wafungue maduka yao na kuendelea na biashara.

“Naomba niwasihi, fungueni maduka hata sasa hivi kama inawezekana wateja wapo, fungueni maduka kwa sababu Kariakoo ni soko la kimataifa tusije kupoteza wateja, pili tunajua kero hizi zinafanywa na watu wetu tuliowapa dhamana, tutawashughulikia,” amesema Majaliwa kwa msisitizo.

Wafanyabiashara hao waliazimia kuanzia leo Jumatatu Mei 15, 2023 wanafunga maduka yao kwa ajili ya kushinikiza Serikali kuingilia kati kuanzishwa kwa sheria na tozo wanazodai zinazowakandamiza ikiwemo zile zinazotaka stoo walizonazo kusajiliwa.

Mgomo huo, umesababisha watu kukosa huduma wakiwemo wafanyabiashara wadogo maarufu kama wachuuzi ambao hufuata bidhaa katika eneo hilo na kusambaza mtaani.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara soko la Kariakoo Martin Mbwana (aliyeshika kipaza sauti) alipokuwa akizungumza na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa sokoni hapo. Picha l Ofisi ya Waziri Mkuu

Maagizo ya Waziri

Pamoja na ombi hilo kwa wafanyabiashara Majaliwa ametoa maagizo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kusitisha mara moja kikosi kazi cha ukusanyaji wa kodi, kusitisha na kuupitia upya utaratibu wa kodi ya ghala pamoja na kuangalia upya utaratibu wa ushuru wa forodha ambao nao umelalamikiwa.

“Tunatambua kuna vikosi kazi vimeundwa kukusanya kodi hapa Kariakoo lakini Rais alishapiga marufuku kwa sababu zinatumika kutesa wafanyabiashara na kuchukua rushwa, hiyo task force isitishwe mara moja, na kama kuna umuhimu wa hicho kitu lazima Waziri wenu wa fedha ajue,” amesema Majaliwa.


Soma zaidi:


Naibu Spika anena

Kwa upande wake Issa Azzan Zungu ambaye ni Mbunge wa Ilala ambako ndipo soko hilo lipo amesema kero zilizopo sokoni hapo zimekuwa zikijirudia mara kwa mara hivyo ni lazima upatikane ufumbuzi wa kudumu.

Aidha, Naibu Spika Zungu ameongeza kuwa wale wote waliohusika kwa kukejeli kauli ya Rais iliyowataka TRA kusamehe kodi za kuanzia miaka mitano iliyopita kwa kuwadai barua rasmi ya tamko hilo wataitwa na kuhojiwa katika kamati ya Bunge na kuchukuliwa hatua.

“Nikuombe wale wote waliokejeli kauli ya Rais kuwa ni siasa sisi tutawaita Dodoma tutawashughulikia, la pili tunawaomba suala la cargo (forodha)  nalo lishughulikiwe, lisitishwe mpaka watakapojipanga,” amesema Zungu.

Wafanyabiashara wakubali Ombi

Licha ya kupongeza hatua hiyo ya Serikali kuitikia wito na kuamua kuzivalia njuga changamoto zao Mwenyekiti wa wafanyabiashara sokoni hapo Martin Mbwana amewaomba wafanyabiashara kuitikia wito wa Serikali wa kufungua maduka yao.

“Kwa kuwa keshokutwa tunakaa kikao, naomba niwatangazie wafanyabiashara tukubali agizo la Waziri Mkuu tumuunge mkono, tufungue biashara zetu, tunaamini baada ya kikao kero zetu zote zitakuwa zimeisha,” amesema Mbwana huku akipigiwa makofi.

Sakata la mgomo wa wafanyabiashara limegonga vichwa vya vyombo vya habari hii leo na kusababisha baadhi ya Wabunge kuomba suala hilo lijadiliwe kwa dharura bungeni ambapo Spika Tulia Ackson aliomba muda ili ajiridhishe.

Baada ya juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla kuwashawishi wafanyabiashara hao kuendelea na shughuli zao kugonga mwamba, Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa taarifa kuwa itakutana na wafanyabiashara hao Mei 17, 2023 katika ofisi za Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo Waziri Majaliwa alifika na kuzungumza na viongozi wa wafanyabiashara kusikiliza kero zao na kisha kuelekea soko la Kariakoo ambako amezungumza na wafanyabiashara hao ana kwa ana na kuahidi kupokea changamoto nyingine Mei 17.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV