BoT yazindua mfumo wa iCBS kuimarisha usimamizi wa masuala ya fedha
- Tanzania nchi ya kwanza Afrika kutengeneza mfumo wa kitaifa wa benki kwa kutumia rasilimali za ndani pekee.
Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua rasmi Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (Integrated Central Banking System) iCBS, mfumo wa kisasa ulioundwa ili kuchochea mageuzi ya usimamizi wa masuala ya kifedha nchini.
Mfumo huu umechukua nafasi ya mfumo wa awali wa Core Banking System (CBS) uliotumika tangu mwaka 1999, na ulianza majaribio mwezi Oktoba 2024 kabla ya kukamilika rasmi Septemba 2024.
Kwa mujibu wa Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, mfumo wa iCBS umezinduliwa baada ya majaribio yaliyothibitisha uimara wake bila changamoto za kiufundi au kiutendaji.
Tutuba amesema mfumo huu umeundwa kufuatia maelekezo ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyesisitiza umuhimu wa mifumo ya Serikali kusomana ili kuongeza ufanisi na kuboresha huduma kwa wananchi.
Hatua hii imeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika kuunda mfumo wa kitaifa wa kibenki kwa kutumia rasilimali za ndani pekee.
Tutuba amesema mfumo wa iCBS umeundwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa sera za fedha na taarifa za kifedha, uchambuzi wa taarifa za miamala kwa wakati halisi, ufuatiliaji wa akiba ya fedha na mapato ya Serikali, pamoja na usimamizi wa riba na mzunguko wa fedha kitaifa.
Pia unatarajiwa kuboresha uwazi kwa wadau wa fedha na taasisi za ndani na nje, kuongeza kasi ya upatikanaji wa taarifa, kupunguza makosa ya kibinadamu na kutoa nafasi ya kufanya maamuzi sahihi kwa kutumia taarifa sahihi na kwa wakati.
Aidha, mfumo huo umeokoa zaidi ya Sh81 bilioni kwa kuepuka ununuzi wa mfumo kutoka nje ambao ulikadiriwa kugharimu Sh91.95 bilioni.
Badala yake, umetumia Sh10.63 bilioni pekee kupitia wataalamu wa ndani, jambo linalothibitisha uwezo mkubwa wa kitaalamu uliopo nchini.
Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, amesema mafanikio haya yamevunja dhana ya kutegemea kila kitu kutoka nje na yamethibitisha uwezo wa Watanzania kufanikisha miradi mikubwa kwa viwango vya kimataifa.
Amesisitiza kuwa mfano huu ufuatwe na wizara na taasisi nyingine kwa kuwekeza katika Tehama na kutumia wataalamu wa ndani ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa ubora wa juu.
Kwa mujibu wa BoT, iCBS ni zaidi ya mfumo wa kiteknolojia ni alama ya uwezo wa kitaifa, uthubutu, na dira ya kujitegemea kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kifedha, huku pia ukihakikisha usalama wa taarifa katika zama za ongezeko la uhalifu wa kimtandao.