BoT yatoa ufafanuzi noti za Tanzania kusambaza virusi vya Corona
- Yasema noti hizo zimetengenezwa kwa namna ya kuweza kuzuia vimelea kusalia kwenye noti.
- Watanzania watakiwa kupuuza taarifa zinazosambaa mtandaoni kuwa noti za fedha za Tanzania zinasambaza virusi vya Corona
- Yawataka wananchi kutumia simu za mkononi, kadi na intaneti kufanya miamala ya fedha.
Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka Watanzania kupuuza taarifa zinazosambaa mtandaoni kuwa noti za fedha za Tanzania zinasambaza virusi vya Corona na imebainisha kuwa noti hizo zimetengenezwa kwa namna inayoweza kuzuia vimelea vya magonjwa kusalia katika noti hizo.
Virusi hivyo ambavyo chimbuko lake ni jimbo la Wuhan nchini China mpaka jana (Machi 18, 2020) kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) vimeua watu 7,807 na watu 191,127 wameambukizwa.
Taarifa iliyotolewa leo na Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki ya BoT imeeleza kuwa noti za Tanzania hazisambazi virusi vya Corona lakini kutokana na kupita katika mikono ya watu wengi, tahadhari ya kujikinga na virusi hivyo zinapaswa kuzingatiwa.
“Benki ya Tanzania inapenda kuutaarifu umma kuwa noti zetu zimetengenezwa kwa namna kuweza kuzuia vimelea kusalia kwenye noti.
“Hata hivyo, kutokana na noti hizo kupita katika mikono ya watu wengi, tunashauri wananchi kuzingatia miongozo inayotolewa na mamlaka zenye dhamana ya afya ya jamii,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Miongozo iliyotolewa na wataalam wa afya ni pamoja na kunawa mikono mara kwa mara, kutumia tishu wakati wa kukohoa, kutokugusa mdomo, pua na macho; na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
Zinahusiana:
Hata hivyo, BoT imesema ili kujiweka salama zaidi wananchi wanaweza kutumia njia mbadala kufanya miamala ikiwemo simu za mkononi, intaneti na kadi bila kulazimika kwenda katika kaunta za benki au mashine za kutolea pesa (ATM) kupata pesa taslimu.
“Tunawasihi wananchi kuwa katika kipindi hiki ambacho Taifa liko katika mapambano dhidi ya COVID-19 kuzipuuza taarifa zinazozagaa mitandaoni ambazo hazina vyanzo vya uhakika, zinazozihusisha noti zetu na usambazaji wa virusi vya corona,” inaeleza taarifa hiyo.