BoT yashikilia CBR 6.25% kudhibiti mfumuko wa bei 

October 8, 2026 3:16 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Uamuzi huo umezingatia athari zinazoendelea ikiwemo vita vya  Mashariki ya Kati na hatari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kubakiza Riba ya Benki Kuu (CBR) katika kiwango cha asilimia 6.25 kwa robo ya nne ya mwaka 2026 ili kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

Hii ni mara ya kwanza Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya BoT inabakiza riba hiyo katika kiwango hicho, ikiwa ni cha juu zaidi tangu taasisi hiyo ianze kutumia mfumo huo Januari 2024. 

CBR ni kiwango cha riba kinachotumiwa na BoT katika shughuli zake za kifedha na benki za biashara na taasisi nyingine za kifedha nchini, hivyo mabadiliko yake huathiri mazingira ya mikopo na ukwasi katika uchumi. 

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amewaeleza wanahabari na vigogo wa taasisi za fedha jijini Dar es Salaam kuwa uamuzi huo umezingatia athari zinazoendelea kutokana na migogoro ya Mashariki ya Kati pamoja na hatari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño. 

Katika kikao chake cha Oktoba 7, 2026, Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya BoT, imesema inatarajia kuwa mfumuko wa bei utaendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5 kwa muda wa kati. 

“MPC inaona kuwa msimamo wa sasa wa sera ya fedha unafaa kwa kuwa unaendelea kutatua athari za kiuchumi, kupunguza shinikizo la msingi la mfumuko wa bei na kukuza ukuaji wa uchumi,” amesema Tutuba. 

CBR ya asilimia 6.25 ilianza kutumika katika robo ya tatu ya mwaka 2026, baada ya BoT kuongeza kiwango hicho kutoka asilimia 5.75 iliyokuwa inatumika katika robo ya pili.

Gavana Emmanuel Tutuba amewaeleza wanahabari na vigogo wa taasisi za fedha jijini Dar es Salaam kuwa uamuzi huo umezingatia athari zinazoendelea kutokana na migogoro ya Mashariki ya Kati pamoja na hatari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño. Picha | Daily News.

Mfumuko wa bei bado ndani ya lengo

Tutuba amebainisha kuwa mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara umeendelea kubaki ndani ya lengo, ingawa umeanza kuongezeka kutokana na kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia.

Kwa mujibu wa Tutuba, mfumuko wa bei ulifikia asilimia 4.3 mwezi Agosti 2026, kutoka wastani wa asilimia 4.1 katika robo iliyoishia Juni 2026, kiwango cha juu zaidi kurekodiwa tangu Aprili 2023. 

“Ongezeko hilo lilichangiwa zaidi na kupanda kwa bei za mafuta duniani kunakotokana na vita vya Mashariki ya Kati, jambo lililoongeza bei za mafuta nchini pamoja na gharama za usafirishaji,” amebainisha Tutuba.

Kwa Zanzibar, mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 5.6 mwezi Agosti kutoka asilimia 6 mwezi Julai, ingawa bado ulikuwa juu ya lengo la muda wa kati la asilimia 5.

Uchumi kukuza kwa zaidi ya 6%

Ukuaji wa uchumi umeendelea kuonyesha maendeleo chanya ukikua kwa asilimia 6 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026 na inakadiriwa kukua zaidi ya asilimia 6 katika robo ya pili na ya tatu kwa Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa Tutuba, ukuaji huo umechangiwa na sekta za huduma za kifedha, uzalishaji viwandani, uwekezaji katika miundombinu na huduma za kijamii.

Kwa upande wa Zanzibar, uchumi ulikuwa kwa asilimia 6.7 katika robo ya kwanza mwaka 2026 na inakadiriwa kukua zaidi ya asilimia 7 katika robo mbili zilizofuata, ikichangiwa na utalii, ujenzi na miradi ya umwagiliaji.

Serikali ya Tanzania inatarajia kuwa uchumi utakuwa kwa asilimia 6.3 mwaka 2026 ukichangiwa na kuimarika kwa shughuli za sekta binafsi. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
30 Oct, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
30 Oct, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
30 Oct, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Tanzania na Angola kuunganisha reli na safari za ndege

Tanzania na Angola kuunganisha reli na safari za ndege

Nukta TV

Tanzania kufungua tena ubalozi Angola, Balozi mpya kuteuliwa

Tanzania kufungua tena ubalozi Angola, Balozi mpya kuteuliwa

Nukta TV

Makonda: 28 - 30 Oktoba ni siku za kumshukuru Mungu kwa kuitunza amani ya Tanzania

Makonda: 28 - 30 Oktoba ni siku za kumshukuru Mungu kwa kuitunza amani ya Tanzania

Nukta TV