Benki ya KCB yaorodhesha hatifungani yake soko la hisa Dar
- Inaitwa Fursa Sukuk inayotii sheria (Shariah) za dini ya Kiislam ambayo ilizinduliwa Novemba 2022.
- Itawawezesha wawekezaji kuombea mkopo kwenye taasisi nyingine za fedha.
- Pia inatoa hakikisho kwa wateja kuwa uwekezaji wao uko salama.
Dar es Salaam. Hatimaye Benki ya KCB imeorodhesha rasmi hati fungani yake ya ‘Fursa Sukuk’ katika Soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) ambayo itawawezesha wawekezaji kuombea mkopo kwenye taasisi nyingine za fedha.
Fursa Sukuk ni hatifungani ya kwanza inayotii sheria (Shariah) za dini ya Kiislam ambayo ilizinduliwa na kuingizwa sokoni Novemba 9, 2022 na haitoi riba bali ni gawio la faida la asilimia 8.75 kwa mwaka.
Upatikanaji wa Fursa Sukuk katika Soko la DSE kunawapa fursa zaidi wawekezaji kwa sababu wataweza kuuza hisa zao kwa wawekezaji wengine (ambao hawajanunua) au kununua hisa kutoka kwa wawekezaji wenza.
“Pia baada ya kuorodhesha hatifungani hii tutaweza kutoa cheti kama uthibitisho ambacho mwekezaji anaweza kukitumia kuombea mkopo kwenye taasisi nyingine za fedha,” imeeleza taarifa ya KCB iliyotolewa Januari 13, 2023.
Hatua hiyo inaashiria kuwa hisa za wateja wa benki hiyo ziko katika mikono salama na wawekezaji wana uhuru wa kusimamia mwenendo wa uwekezaji wao.
Dhumuni ya Fursa Sukuk lilikuwa ni kuchangisha fedha zinazokidhi Shariah kwa kima cha chini cha Sh10 bilioni ambazo zitatumika kufadhili jalada la mali linalozingatia Shariah la ‘KCB Sahl Banking’ inayotoa huduma za kibenki za Kiislamu ikiwemo mikopo, uwekezaji na huduma za miamala za benki.
Fursa Sukuk ilifanikiwa kuvutia uwekezaji wenye thamani ya Sh11 bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 10 ya kiasi kilichotolewa awali cha Sh10 bilioni.
Baadhi ya viongozi wa Benki ya KCB na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) wakiwa katika picha ya pamoja kuashiria kuorodhesha rasmi hati fungani yake ya ‘Fursa Sukuk’ katika Soko la hisa la Dar es Salaam (DSE). Picha | KCB.
KCB yaungana na benki ya NBC
Hatua ya KCB kuorodhesha hatifungani yake katika soko la hisa imekuja zikiwa zimepita zaidi ya wiki tatu baada ya Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kuorodhesha hati fungani yake ya kwanza ya NBC Twiga katika soko hilo.
Hati fungani hiyo ya muda wa kati ya Sh300 bilioni, ilifunguliwa katika soko la awali Oktoba 31, 2022.
Pia hivi karibuni NBC ilitangaza kufunga mauzo ya hati fungani hiyo kwa mafanikio makubwa baada ya kukusanya kiasi cha Sh38.9 bilioni ikilinganishwa na Sh30 bilioni zilizotarajiwa kukusanywa hapo awali. Mafanikio hayo ni asilimia 130 ya malengo yaliyotarajiwa.
Soma zaidi:
Hati fungani ni nini?
Kwa mujibu wa mchambuzi wa masuala ya fedha, Ndahani Mwenda, hatifungani (Bond) ni hati ya deni ambalo Serikali au kampuni hukopa kutokana kwa wawekezaji/umma kwa makubaliano maalum ya kimkataba na huwalipa wawekezaji kwa riba (return coupon) na marejesho baada ya kupevuka (matured) yaani baada ya muda wa makubaliano kufika.
Serikali na makampuni hutoa hatifungani kwa lengo la kupata fedha ya kufanyia shughuli zao. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) huuza hatifungani za serikali kila Jumatano kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kiwango cha riba ni cha ushindani, kama kuna kampuni zaidi ya moja zinazotoa hatifungani na Serikali pia mara nyingi hushindana katika riba ili kuvutia wawekezaji, hivyo kampuni yenye kutoa riba nzuri ndiyo hupata wawekezaji wengi,” ameeleza Mwenda katika moja ya andiko lake lilipo katika mtandao wa Facebook.