Benki ya Dunia yatoa Sh1.1 bilioni kuboresha maisha ya Watanzania
- Fedha hizo ni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kijamii unaolenga kuboresha maisha ya watu wanaoishi katika kaya maskini wakiwemo wanawake na watoto.
- Pia utasaidia kuongeza mahudhurio ya wanafunzi katika shule za msingi na sekondari.
Dar es Salaam. Benki ya Dunia imetoa dola za Marekani milioni 450 sawa na Sh1.1 bilioni kwa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kijamii unaolenga kuboresha maisha ya watu wanaoishi katika kaya maskini wakiwemo wanawake na watoto.
Mradi huo uliopewa jina la “Second Productive Social Safety Net Project (PSSN II)” utatekelezwa na kusimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) ambapo unakusudia kuwafikia Watanzania zaidi ya milioni 5 ambao nusu yao watakuwa ni wanawake.
Fedha hizo zilizotolewa na Benki ya Dunia zitasaidia katika uboreshaji wa matumizi ya chakula na njia za kuishi, kuongeza mahudhurio ya wanafunzi katika shule za msingi; pia upatikanaji wa huduma bora za afya.
Kwa mujibu wa taarifa ya benki hiyo iliyotolewa jana, mradi huo ni muendelezo wa mradi wa kwanza (PSSN II) ambao ulitekelezwa kati ya mwaka 2009 na 2012 katika Wilaya ya tatu za Tanzania na ambao hadi kufikia 2015 ulifanikiwa kuboresha maisha ya kaya takriban milioni moja.
Zinazohusiana:
- Idrisa Magesa: Kijana aliyerithi mikoba ya kuuza uji kutoka kwa bibi yake
- Siku ya Kutokomeza Umasikini Duniani ilivyogeuzwa kuwa Siku ya VICOBA Tanzania
Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia Tanzania, Bella Bird amesema mradi huo utawasaidia wanufaika katika kudunduliza pesa na kupata mali lakini kuokoa maisha ya watu wengi.
“Mradi umesaidia watu wengi katika kutekeleza shughuli nyingi muhimu zikiwemo kuweka pesa pamoja na kupata mali (Assets) nyingine nyingi, hivyo imesaidia kupata chakula kingi zaidi, elimu bora pamoja na afya bora.
“Bado msaada huu utakuwa wenye manufaa kwa watu wengi katika sekta mbalimbali,” amesema Bird.
Tofauti na mradi wa kwanza uliowalenga zaidi vijana lakini huu wa pili unakusudia kuwainua wanawake na watoto kiuchumi na kuwaondolea umasikini katika kaya zao.
Mradi huo unaenda sambamba na mikakati ya Serikali ya kuwaondolea Watanzania umaskini kwa kuboresha miundombinu na huduma za jamii
Latest
