Benki tano zinazoongoza utoaji mikopo ya nyumba Tanzania
- Ni CRDB, Stanbic, Azania, NMB na Benki ya Taifa ya Biashara Afrika (NCBA).
- Zimetoa mikopo kwa wananchi 6,177 yenye thamani ya Sh496.6 bilioni.
- Riba kubwa bado kikwazo kwa watu kuipata mikopo hiyo.
Dar es Salaam. Iwapo una ndoto ya kumiliki nyumba lakini hauna fedha, huenda ukapata mikopo ya kujengea nyumba kutoka benki za biashara Tanzania licha ya kuwa katika baadhi ya taasisi hizo za kifedha utakutana na riba kubwa jambo ambalo ni kikwazo kwa watu wenye kipato kidogo.
Hadi Mei 15, 2022 kwa mujibu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,kulikuwa na benki 32 za Tanzania zilitoa mikopo ya nyumba kwa wananchi 6,177 yenye thamani ya Sh496.6 bilioni.
Ni benki gani ambazo zinatoa mkopo wa nyumba?
Mikopo hiyo, takwimu za wizara zinabainisha kuwa ilitolewa na benki hizo chini ya uwezeshaji ya Kampuni ya Mikopo ya Nyumba ya Tanzania (TMRC) na sehemu kubwa ya mikopo ilitolewa na benki tano za CRDB, Stanbic, Azania, NMB na Benki ya Taifa ya Biashara Afrika (NCBA).
Benki hizo tano kwa pamoja zinamiliki theluthi mbili au asilimia 66.6 ya soko lote la mikopo ya nyumba Tanzania kwa mwaka 2021/22 unaoisha Juni 30.
CRDB ndiyo kinara wa utoaji wa mikopo hiyo ambapo kwa mujibu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetoa mikopo ya nyumba kwa watu 1,653 ikiwa na thamani ya Sh194.3 bilioni.
Kwa mikopo hiyo, CRDB inamiliki soko la mikopo ya nyumba kwa asilimia 39.1 ikiwa katika nafasi ya kwanza Tanzania.
Benki hiyo ya biashara ambayo ni moja ya benki zenye matawi mengi nchini imefuatiwa kwa mbali na benki Stanbic ambayo ilitoa mikopo yenye thamani ya Sh45.9 bilioni kwa wananchi 217 huku ikichuana vikali na Azania ambayo imeshika nafasi ya tatu ikifuatiwa na NMB katika nafasi ya tano ambayo ilitoa mikopo yenye thamani ya Sh30.9 bilioni kwa wananchi 312.
Tano bora ya benki zinazoongoza kutoa mikopo ya nyumba imefungwa na NCBA ambayo ilitoa mikopo kwa wananchi 134 yenye thamani ya Sh24.3 bilioni.
Viwango vya riba vya mikopo ya nyumba hutofautiana kutoka benki moja hadi nyingine kutegemeana na kiwango cha mkopo kinachoombwa na muda ambao mtu anatumia kulipa mkopo husika.
Kuongezeka kwa ushindani wa taasisi za fedha zinazotoa mikopo hiyo kumesaidia kushusha riba kutoka asilimia 22 iliyokuwa inatumika mwaka 2009 hadi asilimia 15 na asilimia 19 mwaka 2021
Kwa nini mikopo ya kujengea nyumba?
Kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2021 kuhusu mikopo ya ujenzi wa nyumba inaeleza kuwa mahitaji ya nyumba nchini yanakadiriwa kufikia nyumba 200,000 kila mwaka ambapo kuna upungufu wa nyumba milioni 3 za makazi ya watu hasa katika majiji makubwa kama Dar es Salaam.
Mahitaji ya nyumba yanachochewa zaidi na ongezeko la idadi ya watu kila mwaka. Hali hiyo ndiyo inayoyafanya benki kutoa mikopo ili kujipatia faida wakati zikirahisisha maisha ya watu kwa kuwawezesha kupata makazi bora ya kuishi.
Mashirika binafsi na umma likiwemo Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) nayo yamejitokeza kuchangamkia fursa ya kujenga nyumba za bei nafuu ambazo hupangishwa au kuuzwa kwa watu.
Kwa mujibu wa TMRC, mwaka 2021 soko la mikopo ya nyumba lilikuwa kwa wastani wa asilimia saba ikilinganishwa na asilimia 6 iliyorekodiwa mwaka juzi.
Soma zaidi:
-
Video: Zingatia haya kabla ya kutafuta nyumba ya kupanga
-
Utafiti: Watanzania hawa wanatamani kumiliki nyumba, shamba lakini hawana fedha
Vikwazo ukuaji wa sekta ya mikopo ya nyumba
Ripoti hiyo ya BoT inaeleza kuwa mahitaji ya nyumba na mikopo ya nyumba bado ni ya juu lakini yanabanwa na uhaba wa usambazaji wa nyumba zinazolingana na viwango vya riba vinavyotozwa katika mikopo ya nyumba.
“Wakopeshaji wengi wanatoa mikopo ya kununua nyumba na kupangisha wakati wachache wanatoa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba binafsi ambapo kwa sehemu kubwa imeendeelea kuwa ni gharama ambayo haiwezi kufikiwa na Watanzania wa kawaida,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
BoT imeeleza zaidi kuwa bado riba za mikopo ya nyumba ziko juu licha ya kuwa zinatozwa kati ya asilimia 15 na 19 na ni wachache wenye uwezo wa kumudu.
“Mchakato mrefu wa utoaji hati za ardhi imeendelea kuwa changamoto inayowaathiri wakopaji kukidhi vigezo vya kupata mikopo ya nyumba,” imeeleza ripoti hiyo.
Hata hivyo, TMRC imesema ili kukuza soko la mikopo ya nyumba kunahitajika jitihada za kuongeza elimu na kupunguza masharti ya kuipata mikopo hiyo ili kuwarahisishia Watanzania wenye nia ya kukopa kuendeleza makazi.
Waziri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina mabula katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2022/23, amesema wataendelea kuratibu utoaji wa mikopo ya ujenzi wa nyumba yenye riba nafuu kutoka taasisi za fedha.
“Pia tutakamilisha miongozo ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na kuisambaza kwa wadau,” alisema Mabula.
Latest
