Bei za petroli, dizeli zaendelea kushuka Tanzania

October 2, 2024 2:13 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Bei ya petroli imeshuka hadi Sh3,011 kwa lita kwa bei ya rejareja jijini Dar es Salaam kutoka Sh3,210 kwa lita iliyokuwa inatumika Julai mwaka huu.

Dar es Salaam. Watumiaji wa vyombo vya moto Tanzania wanaendelea kupata ahueni baada ya bei ya mafuta ya petroli na dizeli kushuka kwa zaidi ya Sh100 kwa lita ndani ya mwezi mmoja, hatua itakayopunguza maumivu kidogo ikilinganishwa na ilivyokuwa miezi mitatu iliyopita. 

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kushuka kwa bei hizo kumechochewa na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na kupungua kwa gharama za uagizaji nishati hiyo muhimu katika kukuza uchumi nchini. 

“Gharama za uagizaji mafuta (Premiums) zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 2.63 kwa petroli na kupungua kwa asilimia 16.58 kwa dizeli na asilimia 3.39 kwa mafuta ya taa katika Bandari ya Dar es Salaam,” imesema taarifa hiyo. 

Kwa mujibu wa bei kikomo zilizotolewa na Ewura bei ya rejareja ya petroli kwa mafuta jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 2 mwaka huu imeshuka kwa Sh129 kwa lita hadi Sh3,011 kwa lita huku dizeli ikiuzwa Sh2,846 kwa lita kutoka Sh3,011 kwa lita mwezi uliopita. Watumiaji wa dizeli wataokoa Sh165 kwa kila lita ikilinganishwa na bei za Septemba 2024.

Ewura imeeleza katika taarifa za bei hizo kuwa petroli itauzwa Sh3,116 kwa lita kwa bei za rejareja katika mikoa ya Mtwara na Tanga. Lita moja ya dizeli kwa bei za rejareja itauzwa Sh2,859 kwa lita mkoani Tanga na Sh2,862 kwa lita huko Mtwara, kusini mwa Tanzania.  

Wakazi wa Dar es Salaam, kwa bei zilizoanza leo, ndiyo watakaonunua petroli kwa bei ya chini zaidi kuliko wote nchini huku wakazi wa Kyerwa Ruberwa mkoani Kagera wakinunua kwa bei ya juu zaidi kwa Sh3,249 kwa lita. 

Kwa bei ya sasa, Sh30,000 jijini Dar es Salaam itakuwa na uwezo wa kununua takriban lita 10 ya petroli kutoka lita 9.53 mwezi uliopita. 

Hii ina maana kuwa gari linalotumia lita moja kwa kilomita 12 sasa litaenda takriban kilomita 120, kilomita tano zaidi kwa kiwango cha mafuta yaliyokuwa yanatumika Septemba 2024, jambo linalookoa gharama kwa watumiaji wa vyombo vya moto wakiwemo bodaboda. 

Hata hivyo, kuendelea kuibuka kwa vita katika eneo la Mashariki ya Kati kati ya Israel na mataifa jirani huenda kukapunguza ahueni hii siku zijazo kutokana na kuathiri mwenendo wa uzalishaji na uchunguzi wa nishati hiyo. 

Enable Notifications OK No thanks