Bei pasua kichwa: Gunia la mahindi lauzwa kwa Sh15,000 Katavi

May 12, 2021 1:26 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Bei ya jumla  imeshuka hadi Sh15,000 katika mji wa Mpanda mkoani Katavi.
  • Bei ya juu kwa sasa ya zao hilo la chakula ni Sh60,000.
  • Serikali yasema itahakikisha wakulima wanapata soko la uhakika la mahindi.

Dar es Salaam. Wakati bei ya mahindi ikiendelea kushuka Tanzania, wakazi wa mji wa Mpanda mkoani Katavi leo Mei 12 ndiyo wananunua zao hilo kwa bei ya chini kabisa kuliko maeneo mengine nchini, jambo ambalo linawaweka wakulima katika wakati mgumu huku likitoa ahueni kwa walaji. 

Kwa mujibu wa ripoti za Mapitio ya Uchumi za kila mwezi (Monthly Economic Review) zinazotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) bei ya zao hilo la chakula imeendelea kushuka kwa miezi minne mfululizo tangu Desemba mwaka jana.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mwezi Novemba 2020 gunia la kilo 100 lilikuwa linauzwa kwa Sh58,012 ambapo bei ikashuka hadi Sh56,892 mwezi uliofuata kabla haijashuka kabisha hadi Sh47,963 mwezi Machi mwaka huu.

Mahindi ni miongoni mwa mazao makuu ya chakula yanayojumuisha mchele, maharage, viazi mviringo, mahindi, mtama, uwele, ulezi na ngano ambayo hutumiwa zaidi na Watanzania.

Hata hivyo, bei hiyo imeendelea kushuka zaidi ambapo takwimu za mazao makuu ya chakula zilizotolewa na Wizara ya Viwanda na Biashara leo (Mei 12, 2021, zinaonyesha wakazi wa mji wa Mpanda wananunua gunia la kilo 100 la mahindi kwa bei ya jumla ya Sh15,000. 

Bei hiyo inayotumika Mpanda ndiyo bei ya chini kabisa kurekodiwa leo sokoni kuliko maeneo mengine ya Tanzania Bara na imedumu katika kiwango hicho hicho kwa wiki mbili mfululizo.


Zinahusiana: 


Wakati Mpanda wakulima na wafanyabiashara wakiuza mahindi kwa Sh15,000, wenzao wa Mwanza wanauza gunia hilo hilo kwa Sh60,000. Bei hiyo ya Mwanza ni mara nne ya inayotumika Mpanda, jambo linalowapa fursa wafanyabiashara kupata faida zaidi na kuwapatia maumivu walaji.

Bei hiyo ya Mwanza ambayo ndiyo bei ya juu kabisa nchini leo (Mei 12, 2021) iko juu kidogo ya wastani wa bei ya kitaifa iliyotumika mwezi Machi mwaka huu ya Sh47,963.

Kushuka kwa bei ya mahindi kunatokana na kuwepo na hifadhi kubwa ya mahindi kwenye maghala iliyosababishwa na kuongezeka kwa mavuno na kutokuwepo kwa soko la uhakika nje ya nchini.

Ili kuhakikisha wakulima wanafaidika na kilimo cha mahindi, Naibu Waziri wa Kilimo amesema Serikali imeanza kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kufanya mazungumzo na mashirika ya kimataifa na nchi jirani ili waweze kununua mahindi ya wakulima. Pia inatoa vibali bure kwa wafanyabiashara waliopata masoko nje ya nchi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW