Balozi Kijazi kuzikwa Tanga, wengi wakimlilia

February 18, 2021 11:57 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Atazikwa Jumamosi Februari 20, 2021 Korogwe, Tanga.
  • Ametajwa kama kiongozi imara, msikivu na mwenye unyenyekevu.
  • Alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma.

Dar es Salaam. Viongozi mbalimbali waliojitokeza kuuga mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi jijini Dodoma, wamemuelezea kwa sifa mbalimbali ikiwemo unyenyekevu na uwezo wake wa kusikiliza na kutatua changamoto zinazojitokeza  kwenye jamii. 

Dk Kijazi alifariki  Februari 17, 2021 Saa 3 usiku katika hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu, kwa kwa mujibu wa taarifa ya Rais John Magufuli iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa.

Leo mwili wake umeagwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) jijini Dodoma ambacho alikuwa Mkuu wa Chuo hicho. 

Katibu Mkuu Ikulu, Dk Moses Kasiluka amesema baada ya mwili wa marehemu kuagwa UDOM unasafirishwa hadi jijini Dar es Salaam na kesho Februari 19, 2021 utaagwa kwa ibada katika viwanja vya Karimjee jijini humo ikiongozwa na Rais John Magufuli pamoja na viongozi wengine. 

Baada ya ibada hiyo, Dk Kijazi atasafirishwa hadi katika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga ambapo atapumzishwa katika nyumba yake ya milele siku ya Jumamosi Februari 20 mwaka huu. 

Viongozi waliojitokeza wakati wa kuuga mwili wa marehemu Dk Kijazi jijini Dodoma wamesema wataendelea kumuenzi kiongozi huyo kwa mazuri yake aliyofanya katika utumishi wa umma. 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Bilinith Mahenge amesema Taifa limepoteza hazina kubwa ikizingatiwa kuwa marehemu alikuwa na uwezo mzuri wa kiuongozi wa kusimamia shughuli za Serikali hasa zile zilizokuwa katika majukumu yake.

“Tumepoteza hazina kubwa kwa Taifa,” amesema Dk Mahenge wakati akitoa salamu zake wakati wa kuaga mwili wa marehemu. 

Amesema atamkumbuka Balozi Kijazi alivyosimamia mchakato wa Serikali kuhamia Dodoma ambapo alisimamia vizuri vikao na kutoa maelekezo mahususi yaliyofanikisha jambo hilo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akitoa heshima za mwisho mbele ya jeneza la Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi. Picha|Mtandao.

Viongozi wengine wamemtaja Balozi Kijazi kama mtu aliyekuwa na uwezo kuwaongoza wengine kivitendo na kuonyesha njia ili kutatua changamoto  mbalimbali za kijamii.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema siku za uhai wake marehemu aliwasisitiza zaidi watumishi wa umma kuzingatia maadili ya kazi  zao ili kuwahudumia wananchi vizuri.

Amewataka wananchi kuendelea kumuenzi kiongozi huyo kwa vitendo hasa katika nyanja ya kutoa mwelekeo mzuri wa kiuongozi. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Alphonce Chandika amesema marehemu alikuwa msikivu na asiyejikweza kutokana na cheo alichokuwa nacho.

“Alikuwa msikivu kwa maelekezo yote tuliyokuwa tukimpatia na dawa zote tulizokuwa tukimpatia alikuwa hahoji chochote kuonyesha yeye ni kiongozi mkubwa anayestahili kutibiwa mahali pengine,” amesema Dk Chandika akielezea namna ambavyo marehemu alivyokuwa msikivu wakati akipata matibabu hospitalini hapo kabla ya mauti hayajamkuta. 

Balozi Kijazi ambaye alikuwa na Shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa Umma na  Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara Kuu kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza amewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini India, Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal kati ya mwaka 2007 hadi 2016.


Soma zaidi:


UDOM wapoteza nguzo muhimu

Licha ya kuwa Balozi Kijazi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi pia alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)  tangu Desemba 2020 aliyechukua nafasi iliyoachwa na hayati Rais mstaafu Benjamin Mkapa. 

Kabla ya kifo chake, alifanikiwa kusimamia mahafali  ya 11 ya chuo hicho ambayo yalifanya vitu vikubwa vitatu: kumsimika yeye kama Mkuu wa Chuo wa pili wa Chuo Kikuu Cha Dodoma, lakini pili mahafali hayo  yalimtunuku Rais mstaafu marehemu Mkapa aliyekuwa Mkuu wa Chuo wa kwanza shahada ya heshima ya udaktari wa kifalsafa.

Kutokana na kifo hicho, uongozi wa chuo hicho umesema umempoteza kiongozi makini aliyekuwa na mwenye maono makubwa ya kukiimarisha na kukikuza chuo hicho kitaaluma. 

Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Faustine Bee amesema katika muda mfupi alihudumu katika nafasi yake katika chuo hicho, marehemu Kijazi alikuwa mtu anayesikiliza, anayeshauri, anayeelekeza na ambaye alitamani sana kukiendeleza chuo hicho.

“Alitamani kuona Chuo Kikuu cha Dodoma kinakua kipya, haki na wajibu bila ubaguzi wa aina yoyote unatawala. Alipenda kuona Watanzania wanakimbilia chuo hichi kusoma na kufanya kazi,” amesema Profesa Bee. 

Balozi Mhandisi John Kijazi ameacha mjane na watoto watatu.

Enable Notifications OK No thanks