Bajeti Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge yafikia Sh782 bilioni mwaka 2025-26
- Itajumuisha shughuli zote ndani ya ofisi ya waziri mkuu na mfuko wa Bunge.
- Sh249 bilioni yaongezeka zaidi ikilinganishwa na fedha iliyoombwa mwaka 2024/25.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameliomba Bunge kuidhinisha Sh782 bilioni kwa ajili ya matumizi ya ofisi yake pamoja na Bunge katika mwaka wa fedha wa 2025/26 ikiwa ni ongezeko la Sh249 bilioni iliyoombwa kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Majaliwa, aliyekuwa akisoma hotuba ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2024/2025, amewaambia wabunge kuwa kati ya fedha hizo zilizoombwa, Sh595 bilioni ni kwa ajili ya ofisi yake pamoja na taasisi zilizopo chini yake.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2025/2026, Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake inaliomba Bunge lako tukufu liidhinishe jumla ya shilingi bilioni 595,291,624,000 kati ya fedha hizo, shilingi 183,821,010,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 411,470,614,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.” amesema Majaliwa bungeni jijini Dodoma leo, Aprili 9, 2025 .
Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa fedha zilizoombwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika ofisi ya waziri mkuu ni asilimia 69.11 ya Sh595 bilioni ambapo fedha nyingine zitatumika katika matumizi ya kawaida ikiwemo kulipa mishahara.

Bunge kutengewa mabilioni
Aidha, Majaliwa ameliomba Bunge kuidhinisha Sh186.7 bilioni kwa ajili ya mfuko wa Bunge ambapo Sh 174.9 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh11.7 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Katika fedha hizo zilizoombwa kwa ajili ya mwaka wa 2025/26 kuna ongezeko la Sh4.9 bilioni kulinganisha na fedha iliyoombwa na ofisi ya waziri mkuu kwa ajili ya mfuko wa bunge kwa mwaka 2024/25 ambayo ni Sh 181.8 bilioni.
Mwaka 2022/23 Ofisi ya Waziri Mkuu iliomba kuidhinishiwa Sh532.7 bilioni ambapo Sh350.9 bilioni zilikuwa kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake na Sh181.8 bilioni zilikuwa kwa ajili ya Ofisi ya Bunge.
Kiasi cha Sh244 bilioni kimeongezeka katika fedha inayoombwa na Ofisi ya Waziri Mkuu huku Sh4.9 bilioni ikiongezeka katika fedha iliyoombwa kwa ajili ya mfuko wa Bunge.
Pamoja na Sh4.9 bilioni kuongezeka katika fedha iliyoombwa kwa ajili ya mfuko wa Bunge, fedha za maendeleo chini ya mfuko huo imeongezeka kwa Sh2 bilioni, kutoka Sh9.68 bilioni kwa mwaka 2024/25 hadi Sh11.79 bilioni kwa mwaka 2025/26.

Undani wa bajeti kugharamia miradi ya maendeleo
Uchambuzi wa Nukta Habari umebaini kuwa Sh 423 bilioni sawa na asilimia 54.12 ya fedha zilizoombwa ndiyo zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo katika Ofisi ya Waziri Mkuu na mfuko wa Bunge. Kiasi hicho cha bajeti ya maendeleo ni zaidi ya nusu ya bajeti nzima iliyoombwa na Majaliwa.
Huenda jambo hilo limechochewa na matukio ya majanga yaliyotokea hivi karibuni, yakiwemo ajali na maafa kama lile la kuporomoka kwa jengo la ghorofa Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Kwa kuwa idara ya masuala ya majanga na uokozi ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, hivyo kuifanya serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kuona umuhimu wa kuongeza fedha kwa ajili ya maandalizi na utatuzi wa haraka wa majanga yanapojitokeza.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ameeleza kuwa moja kati ya sababu zilizopelekea kuongezeka kwa Bajeti katika pendekezo hilo ni kupanda kwa bei za bidhaa.
Latest



