Bajeti Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge yafikia Sh339 bilioni mwaka 2023-24
- Itajumuisha shughuli zote ndani ya ofisi ya waziri mkuu na mfuko wa Bunge.
- Sh58 bilioni yaongezeka zaidi ikilinganishwa na fedha iliyoombwa mwaka 2022/23.
- Asisitiza halmashauri kukusanya mapato na kukemea vitendo vilivyo kinyume na maadili.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameliomba Bunge kuidhinisha Sh339 bilioni kwa ajili ya matumizi ya ofisi yake pamoja na Bunge katika mwaka wa fedha wa 2023/24 ikiwan ni ongezeko la Sh58 bilioni iliyoombwa awali kwa mwaka huu wa fedha.
Majaliwa, aliyekuwa akisoma hotuba ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024, amewaambia wabunge kuwa kati ya fedha hizo zilizoombwa, Sh173.7 bilioni ni kwa ajili ya ofisi yake pamoja na taasisi zilizopo chini yake.
“Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake inaliomba Bunge lako liidhinishe jumla ya Sh 173.7 bilioni kati ya fedha hizo Sh 121.4 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh52.4 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo,” amesema Majaliwa bungeni jijini Dodoma leo, Aprili 5, 2023 .
Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa fedha zilizoombwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika ofisi ya waziri mkuu ni asilimia 30 tu ya Sh 173.7 bilioni ambapo fedha nyingine zitatumika katika matumizi ya kawaida ikiwemo kulipa mishahara.
Bunge kumwagiwa mabilioni
Aidha, Majaliwa ameliomba Bunge kuidhinisha Sh165.6 bilioni kwa ajili ya mfuko wa Bunge ambapo Sh160.4 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh5.2 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Katika fedha hizo zilizoombwa kwa ajili ya mwaka wa 2023/24 kuna ongezeko la Sh58 bilioni kulinganisha na fedha iliyoombwa na ofisi ya waziri mkuu mwaka 2022/23 ambayo ni Sh 281 bilioni.
Soma zaidi
- Tanzania yasema hakuna maambukizi mapya ya Marburg
- Ifahamu mikoa 3 yenye watoto wengi waliodumaa Tanzania
- Sheikh wa mkoa Mwanza: Serikali idhibiti muda watoto kurudi nyumbani
Mwaka 2022/23 Ofisi ya Waziri Mkuu iliomba kuidhinishiwa Sh281 bilioni ambapo Sh148.9 bilioni zilikuwa kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake na Sh132.7 bilioni zilikuwa kwa ajili ya Ofisi ya Bunge.
Kiasi cha Sh25 bilioni kimeongezeka katika fedha inayoombwa na Ofisi ya Waziri Mkuu huku Sh33 bilioni ikiongezeka katika fedha iliyoombwa kwa ajili ya mfuko wa Bunge.
Pamoja na Sh33 bilioni kuongezeka katika fedha iliyoombwa kwa ajili ya mfuko wa Bunge, fedha za maendeleo chini ya mfuko huo imepungua kwa Sh231 milioni, kutoka Sh5.4 bilioni mwaka 2022/23 hadi Sh5.16 bilioni kwa mwaka 2023/24.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya 2023/2024, bungeni jijini Dodoma, Aprili 5, 2023. Wengine kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Wziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Patrobas Katambi.PichalOfisi ya Waziri Mkuu
Humusi ya bajeti kugharamia miradi ya maendeleo
Uchambuzi wa Nukta Habari umebaini kuwa Sh 57.6 bilioni sawa na asilimia 17 ya fedha zilizoombwa ndiyo zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo katika Ofisi ya Waziri Mkuu na mfuko wa Bunge. Kiasi hicho cha bajeti ya maendeleo ni sawa na humusi au moja ya tano ya bajeti nzima iliyoombwa na Majaliwa.
Kwa miaka kadhaa sasa baadhi ya wadau wamekua wakiikosoa vikali Ofisi ya Waziri Mkuu juu ya namna inavyokabiliana na maafa nchini ikiwemo matumizi ya vifaa duni katika uokoaji.
Novemba 2022 baadhi ya wadau waliikosoa ofisi hiyo wakituhumu kuwa iwapo uokoaji ungefanywa inavyotakiwa wakati wa ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea Bukoba basi watu wengi zaidi wangesalimika.
Hata hivyo, leo Majaliwa amesema katika mwaka 2022/23 amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na maafa ikiwemo kutoa mafunzo kwa wajumbe 555 wa Kamati za Usimamizi wa Maafa na Waratibu wa Maafa kuimarisha uwezo wa utendaji kazi katika mikoa ya Arusha, Morogoro, Kilimanjaro, Lindi, Mtwara na Singida.
Wavuvi zaidi ya 300 wapewa mafunzo ya uokoaji
“Pia, wavuvi 344 katika mwambao wa Ziwa Victoria na vijana 40 wa kujitolea katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Songwe na Tabora walipata mafunzo ya uokoaji, yaliyowaongezea uwezo wa kukabiliana na maafa kwa wakati,” amesema.
Katika hotuba yake, Majaliwa amezitaka halmashauri nchini kusimamia ipasavyo makusanyo ya kodi huku akikemea vikali vitendo visivyo na maadili. Pia, kiongozi huyo amezitaka halmashauri kutumia vema takwimu za sensa ya watu na makazi pamoja na kutenga fedha za tathmini ya maendeleo.
Latest



