Tanzania yasema hakuna maambukizi mapya ya Marburg

April 4, 2023 12:22 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Idadi ya visa yasalia nane huku waliofariki dunia wakisalia watano.
  • Mmoja aruhusiwa baada ya kubainika  hana tena virusi hivyo.
  • 35 waliotengwa waruhusiwa mara baada ya kumaliza siku 21 za uangalizi malaumu.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema hakuna maambukizi mapya ya ugonjwa wa Marburg yaliyorekodiwa siku za hivi karibuni zaidi watu wanane waliombukizwa hapo awali huku watu 35 kati ya 212 waliokuwa chini ya uangalizi maalumu wakiruhusiwa kurejea makwao.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewaeleza wanahabari jijini Dar es Salaam leo (Aprili 4, 2022) kuwa hadi sasa ugonjwa huo bado haujasambaa zaidi ya kata mbili za Wilaya ya Bukoba ulipo ripotiwa hapo awali.

“Hadi leo Aprili 4, 2023 jumla ya visa vya watu waliothibitika kuwa na ugonjwa wa Marburg vimebaki kuwa ni vilevile nane na vifo vitano. Ni jambo la kumshukuru mwenyezi Mungu kuwa hatujapata visa vipya wala kifo kipya,” amesema Ummy.

Pamoja na kutokuongezeka kwa idadi ya visa vya Marburg, Ummy amesema leo madaktari wamemruhusu mgonjwa mmoja aliyekuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa huo baada ya kujiridhisha kuwa hana tena virusi hivyo.

“Leo tumemruhusu mgonjwa mmoja, mwanaume mwenye umri wa miaka 26, akiwa na afya njema na hana Virusi vya Marburg, ni matumaini yangu kuwa jamii itampokea vyema na kushirikiana nae kwenye shughuli zake za kila siku,” amesema Ummy.

Waziri Ummy ametoa rai kwa jamii kutomnyanyapaa mgonjwa huyo ikiwa ni pamoja na watu wengine 35 ambao nao wameruhusiwa baada ya kumaliza muda wao wa uangalizi maalumu.


Soma zaidi


35 waruhusiwa kutoka ‘quarantine’ 

Watu hao 35 walioruhusiwa ni kati ya 212 ambao waliwekwa chini ya uangalizi maalumu kwa siku 21 mara baada ya kubainika waliingiliana kwa namna moja au nyingine na wagonjwa au marehemu waliofariki kwa ugonjwa huo.

Ummy ametumia mkutano huo na wanahabari kuwahakikishia Watanzania pamoja na jumuiya za kimataifa kuwa Wilaya ya Bukoba pamoja na Mkoa wa Kagera ni salama hivyo watu waendelee na shughuli zao kama kawaida.

“Ninawahakikishia pasi na shaka kuwa, Bukoba ni salama, Kagera ni salama na Tanzania ni salama hivyo tuendelee na shughuli na safari zetu bila hofu yoyote,” amesisitiza Ummy.

Itakumbukwa tarehe 21 mwezi March 2023, Serikali ilitangaza uwepo wa mlipuko wa Marburg katika Kata mbili za Maruku na Kanyangereko zilizopo wilayani Bukoba katika mkoa wa Kagera ikiwa imepita siku tano tangu mlipuko huo utokee.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ugonjwa huo uliripotiwa kwa mara ya kwanza nchini Ujerumani mwaka 1967 mjini Marburg na baadaye uliripotiwa katika nchi mbalimbali barani Afrika baadae.

Inashauriwa kuepuka kugusa vimiminika kutoka kwa mgonjwa wa Marburg kama kinyesi, mkojo, matapishi jasho au damu kutogusa vitu vilivyotumiwa na mgonjwa wa maradhi hayo pamoja na kuepuka kugusa au kula mizoga ya wanyama kama popo, nyani, na swala wa porini.

Enable Notifications OK No thanks