Baada ya ‘kifungo’, Mpina aendelea kuwasha moto bungeni
- Ataka mikataba yote ya rasilimali kuletwa bungeni ili ipitiwe na wabunge.
- Mwigulu amtaka afute kauli, afuta huku akiendelea kuwa “wa moto”.
Dar es Salaam. Baada ya kumaliza adhabu ya kutohudhuria vikao 15 vya Bunge, Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, leo ameibua tena mjadala mkali kuhusu suala la kampuni ya DP World kutoza kodi katika Bandari ya Dar es Salaam licha ya kuwa mwekezaji.
Mpina, ambaye alihukumiwa kwa kutoa tuhuma za uongo dhidi ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, sasa anadai mikataba ya rasilimali kama ile ya bandari inapaswa kuletwa bungeni kwa uwazi.
Akichangia hoja ya Kamati ya Mipango leo Novemba 7, 2024, bungeni jijini Dodoma, Mpina amehoji kwa nini mwekezaji huyo ameanza kukusanya kodi, akidai kwamba licha ya uwekezaji wa Dola milioni 250 (takriban Sh687 bilioni) uliopangwa kufanywa na DP World ndani ya miaka mitano, tayari kampuni hiyo inadaiwa kukusanya mapato.
Mpina bado wamoto bungeni.
“Waziri hapa anaeleza kuwa mwekezaji wa DP World atawekeza Dola za Marekani milioni 250, lakini tayari muwekezaji huyo ameshaenda anakusanya kodi sasa,” amesema Mpina.
Mpina, aliyewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi katika Serikali ya hayati Rais John Magufuli, ndani ya miaka miwili amekuwa akitumia vikao vya Bunge na mikutano ya wanahabari kuikosoa Serikali kwenye masuala mbalimbali yakiwemo ya kilimo na uchumi.
Kutokana na umachachari wake, mnamo Julai 24, mwaka huu, Bunge chini ya Spika Tulia Ackson lilimsimamisha Mpina kuhudhuria vikao 15 kwa tuhuma za kusema uongo na kukiuka kanuni za Bunge.
Hata baada ya kurejea kutoka “kifungoni”, leo mbunge huyo amehoji ni kwa nini Serikali inashindwa kupeleka mikataba bungeni ili wabunge waweze kujadili makubaliano yaliyopo, akirejelea Sheria ya Rasilimali Asili, kifungu cha 12, kinachotaka mikataba yote ya rasilimali kupitiwa bungeni.
“Naendelea kuuliza hivi imeshindikana nini kuleta mikataba ya Bandari ya Dar es Salaam tulioingia na DP World hapa bungeni? Nani aliyeenda kukubali kwamba sisi tunakubali uwekezaji wa Sh687 bilioni? Nani aliyeenda kukubali kwamba tumekubali ‘ratio’ ya kugawana mapato na DP World kwa ‘ratio’ ya 40/60,” amehoji Mpina.
Mpina akichangia hoja Bungeni leo baada ya kutoka “kifungoni” ikiwa ni miaka miwili sasa toka aanze kuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali kwa kutumia vikao vya Bunge na mikutano ya wanahabari. Picha/Jamhuri Media.
Mwigulu amtaka afute kauli.
Muda mfupi baada ya kauli hiyo ya Mpina, Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisimama na kumtaka Mpina kufuta kauli yake kuhusu DP World kukusanya kodi au kutoa ushahidi wa kauli hiyo.
Kanuni ya 70(3) ya Bunge inaruhusu mbunge mwingine kusimama na kuomba utaratibu iwapo anaamini kuwa kauli ya mbunge aliyezungumza awali ni ya uongo au inakinzana na maelezo sahihi kuhusu jambo linalojadiliwa Bungeni.
Waziri Nchemba amesisitiza kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pekee ndiyo yenye mamlaka ya kukusanya kodi nchini na kwamba DP World haihusiki na ukusanyaji wa tozo hizo.
“Nathibitishia Bunge lako tukufu kwamba hakuna kodi yoyote inaruhusiwa kukusanywa na taasisi isiyo ya Serikali au ambayo haijapewa mamlaka hiyo. Hakuna kodi yoyote ambayo DP World inakusanya,” amesema Waziri Nchemba kwa uwazi.
Baada ya Mwigulu kueleza hivyo, Mpina alisimama na kufuta kauli yake licha ya kueleza baadhi ya mambo katika maelezo yake ya awali.