Esau Ng’umbi wa Nukta Africa kuwania tuzo Samia Kalamu Awards

November 12, 2024 1:40 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Tuzo ya habari za mifugo na uvuvi na tuzo ya fedha na uchumi.
  • Hii ni mara ya tatu ndani ya mwaka 2024 Esau kuwania tuzo mbalimbali.

Dar es Salaam. Mwanahabari kutoka Kampuni ya Habari na Teknolojia ya Nukta Africa kwa mara nyingine amechomoza katika wateule wa tuzo za Samia Kalamu Awards zilizoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)  kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa HabariWanawake Tanzania (TAMWA).

Tuzo hizo zenye kaulimbiu “Uzalendo Ndio Ujanja” zimegawanywa katika makundi makuu matatu ambayo ni tuzo maalumu za kitaifa, tuzo za vyombo vya habari na tuzo za kisekta ambapo Ng’umbi anawania tuzo mbili katika kundi hili ambazo ni tuzo ya mifugo na uvuvi na tuzo ya fedha na uchumi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa Tamwa Dk Rose Reuben na Mkurugenzi wa TCRA Dk Jabir Bakar kazi 85 zilizoteuliwa kutoka kazi 1,131 zilizowasilishwa zitapigiwa kura na wananchi ambao ndio walaji wa habari ambapo maamuzi yao yatachangia upatikanaji wa mshindi kwa asilimia 60 huku uamuzi wa majaji ukiwa na asilimia 40.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa zoezi la upigaji kura limeanza jana Novemba 11, 2024 na litamalizika Novemba 20 mwaka huu ambapo tuzo zinatarajiwa kutolewa Desemba 10, 2024.

Unaweza kupiga kura kupitia tovuti ya www.samiaawards.tz ambapo utaona orodha ya kazi zinazoshindanishwa kwenye sehemu iliyoandikwa “piga kura” mara baada ya kufanya uchaguzi wa makundi ya tuzo, hakikisha unachagua namba ya mshiriki kwa kuangalia picha na kazi aliyochapishwa na ukisharidhika bofya neno piga kura na hapo utakuwa umemchagua mshindi unayemtaka.

Aidha, unaweza kupiga kura kupitia simu ya kiganjani kwa kutuma ujumbe wa kawaida wenye neno “kura”, acha nafasi, kisha weka namba ya mshiriki na tuma kwenda 15200 ambapo utapokea ujumbe mfupi kuthibitisha umefanikiwa kupiga kura.

Hata hivyo, ili uweze kupiga kura kupitia njia ya ujumbe mfupi wa maandishi inatakiwa uwe na angalau Sh100 kwenye salio la kawaida.

Itakumbukwa kuwa hii ni mara ya tatu kwa Ng’umbi kuingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo kwa mwaka 2024, ambapo Septemba 28, 2024 alishinda tuzo ya Umahiri katika Uandishi wa Habari za Madini huku akiibuka mshindi wa pili katika tuzo za elimu na mshindi wa tatu kwenye tuzo za uchumi na biashara na Novemba 2, alipata cheti kwa kuwa mshindi wa pili kwenye tuzo za uadilifu katika taaluma ya habari zinazotolewa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).

Ng’umbi ambaye kwa sasa ni mratibu wa shughuli za dawati la habari Nukta Afrika amesema kuwania tuzo hizo ni matunda ya kufanya kazi zinazogusa jamii kwa kuwa na matokeo chanya huku akiwataka wanahabari hususan wa vyombo vya mtandaoni kutumia majukwaa yao kufanya kazi zenye tija kwa jamii na zinazoweza kuchochea jamii kufanya maamuzi sahihi.

“Kwanza imenitia moyo kwa kazi yangu kutambulika kuwa ina mchango chanya katika kuleta mabadiliko kwenye jamii, imenitia ujasiri wa kuendelea kuandika habari zinazogusa jamii na kuwasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi. 

Aidha ni deni na ukumbusho kwa waandishi wa habari za mtandaoni kuwa tunaweza kutumia majukwaa ya kidijitali kubadili maisha ya watu, uandishi wa habari za mtandaoni si kuhusu udaku pekee,” amesema Ng’umbi.

Enable Notifications OK No thanks