Arusha yaweka mikakati kuboresha miundombinu kuelekea AFCON 2027
- Serikali yaahidi kuboresha barabara,na vifaa vya usalama, njia bora za usafirishaji wa mashabiki na timu.
Arusha. Jiji la Arusha limejipanga kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara ili kuvutia wageni watakaokuja katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Mashindano ya AFCON yanayotarajiwa kufanyika mwaka 2027 katika nchi za Tanzania , Kenya na Uganda yanatajwa kuwa miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii nchini.
Kutokana na umuhimu wa mashindano hayo Serikali ilianza maboresho ya viwanja vya michezo vilivyopo pamoja na ujenzi wa uwanja mpya wa michezo jijini Arusha ambao ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 60.
Mbali na ujenzi wa uwanja huo Mkuu wa Wilaya ya Arusha Joseph Mkude amesema wanatarajia kukarabati miundombinu mbalimbali ya jiji hilo ikiwemo barabara kwa ajili ya kuvutia wageni.
“ Tayari mkakati na mchoro upo mipango miji kuhakikisha barabara zinapitika kuelekea viwanja vya michezo…
…Tumeshaanza mikakati ya kuwa na mabango na matangazo ya AFCON maeneo yote ya jiji lakini pia kuwa na nembo na kaulimbiu ya Arusha kwa AFCON,” amesema Mkude aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Septemba 23, 2025.
Kwa mujibu wa Mkude miundombinu mingine itakayoongezwa ni pamoja na vifaa vya usalama, njia bora za usafirishaji wa mashabiki na timu,taa za barabarani, bendera, sanaa ya mitaani na mapambo ya kiutamaduni.
Huenda ukarabati na maboresho hayo yanayotarajiwa kufanyika katika jiji hilo hususan maeneo ya pembezoni ambayo yanakabiliwa na ubovu wa miundombinu kwa kiwango kikubwa ukaongeza mvuto wa jiji hilo la kitalii.
Pamoja na miundombinu hiyo Mkude amesema watadhibiti takataka zinazozagaa hovyo mitaani kwa kuanzisha utaratibu wa kuzirejereza huku akiahidi uboreshaji wa masoko na vituo vya daladala ambavyo vyote vitaenda kuboresha jiji la Arusha.
Aidha, Mkude amesema watawachukulia hatua wale wote wanaohujumu miundombinu ya barabara na mwananchi atakayefanikisha kukamatwa kwa wahujumu hao wa miundombinu atazawadiwa Sh500,000.