Alichokisema Majaliwa akiwanadi wagombea wa CCM Ruangwa
- Awataka Wananchi kuwapigia kura wagombea wa CCM ili wawaletee maendeleo.
Arusha. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Wananchi wa Ruangwa mkoani Lindi kuwapigia kura wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ili kuendeleza shughuli za maendeleo zilizokuwa zikifanywa mkoani humo.
Majaliwa ameyasema hayo wakati akimnadi mgombea wa nafasi ya Urais, ubunge na udiwani kwa tiketi ya CCM katika jimbo la Ruangwa mkoani Lindi leo Septemba 24, 2025 akisisitiza kuwa baadhi ya miradi ya maendeleo mkoani humo haiwezi kukamilika bila Samia Suluhu Hassan kushinda nafasi ya Urais.
“Tuna miradi inayoendelea kwenye mkoa huu wewe (Samia Suluhu Hassan) umeanzisha ujenzi wa bandari ya uvuvi kule Kilwa inaendelea kujengwa na haiwezi kukamilika bila wewe mwenyewe kuukamilisha mradi huo…
…Wanaruangwa, wanalindi mnajua barabara yetu ya Lindi – Kibiti imeharibika kidogo mheshimiwa Rais alishaanza kujenga madaraja makubwa kwenye maeneo yote,” amesema Majaliwa.
Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo kuzungumza katika jimbo hilo aliloliongoza kwa miaka 15 baada ya kutangazwa rasmi kuwa hatogombea ubunge katika jimbo hilo kwa miaka mitano ijayo.
Uamuzi wa Majaliwa huo ulitangazwa Julai 2, 2025 na Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ruangwa, Mkoa wa Lindi, Abbas Makwetta.
Kwa sasa bendera ya CCM jimbo la Ruangwa inapeperushwa na Kaspar Mmuya ambapo Majaliwa amewataka wananchi hao kumuunga mkono ili aweze kuwaletea maendeleo.
“Niliwaambia mimi pamjoa na nyie tutaendelea kumpa ushirikiano mheshimiwa Kaspard Mmuya ambaye ameanza kazi ya kupita kwenye maeneo yenu na kuhakikisha kwamba atafanya kazi na kushirikiana na nyie.” ameongeza Majaliwa.
Kwa upande wake mgombea Urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan amemshukuru Majaliwa kwa kuja kuongeza hamasa za Wananchi wa eneo hilo huku akihidi maendeleo mkoani humo ikiwemo kuboresha miundombinu ya umeme
‘Tumetanguliza umeme wa kutosha ili tuje tuweke kongani ya viwanda…Niwaahidi kuwa kazi bado ipo na kazi tunakuja kuifanya,” amesema Samia.
Pamoja na hayo amewaahidi wananchi hao ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mtwara hadi Mbambabay, kuboresha sekta ya madini, pamoja na kukabiliana na wanyama vamizi.
Latest
