Ajali za barabarani zimepungua kwa asilimia 33.8-Jeshi la Polisi

January 22, 2019 10:00 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka 2018, kulitokea matukio 3,978 ya ajali za barabarani ukilinganisha na matukio 6,022 yaliyotokea mwaka uliotangulia wa 2017.
  • Matukio ya watoto kupotea, mauaji yaliyotokana na ulevi nayo yamepungua.
  • Wananchi watakiwa kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limesema kuimarika kwa utekelezaji wa sheria na kampeni za kudhibiti uhalifu kumesaidia kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia 33.8 mwaka 2018. 

Sambamba na hilo ni kupungua kwa matukio ya kupotea kwa watoto kutoka matukio 134 mwaka 2017 hadi 116 mwaka uliopitaambapo wazazi wametakiwa kuchukua tahadhari ya kuwalinda watoto popote walipo.

Akitoa taarifa ya uhalifu kwa mwaka 2018 leo (Januari 21, 2019) jijini Dar es Salaam, Msemaji wa jeshi hilo, Ahmed Msangi amesema kwa ujumla uhalifu umepungua nchini kutokana na kuimarika kwa kampeni na juhudi za pamoja za wadau wa amani kupambana na uhalifu wa aina mbalimbali. 

Amesema katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka 2018, kulitokea matukio 3,978 ya ajali za barabarani ukilinganisha na matukio 6,022 yaliyotokea mwaka uliotangulia wa 2017. 

Hiyo ina maana kuwa ajali zimepungua kwa asilimia 33.8 au upungufu wa ajali 2,034. 

“Kupungua matukio ya uhalifu nchini na ajali za barabarani kunaonyesha wazi kwamba zipo juhudi za Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya amani kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu, mafanikio ya kampeni mbalimbali zinazoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi nazo zimekuwa ni chachu ya vita dhidi ya uhalifu,” amesema Msangi. 

Ajali za barabarani hupunguza nguvu kazi ya Taifa na kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi. Picha| dzbreaking.com

Pia mauaji yaliyotokana na ulevi yamepungua kutoka 129 mwaka 2017 hadi 118 mwaka uliofuatia. 

Hata hivyo, Msangi ambaye alikuwa akizungumza mbele ya Wanahabari amewataka watumiaji wa vilevi kunywa kwa kiasi na kujiepusha na vitendo vya fujo wanapokuwa wamelewa.

Wananchi na watumiaji wa vyombo vya moto vya usafiri watakiwa kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuwahakikishia usalama wao.


Zinazohusiana:


Kukua kwa uchumi na kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara na kipato kwa baadhi ya Watanzania kumeongeza vyombo vya moto vya usafiri. Hali hiyo imesababisha kuwepo kwa ajali za barabarani ambazo siyo tu zimesababisha upotevu wa nguvu kazi, lakini pia kuongeza uharibifu wa miundombinu na mali, na kusababisha vifo na majereha kwa manusura.

Sababu zinazochangia ajali za barabarani zimetajwa kuwa ni sababu za kibinadamu, uchakavu au ubovu wa vyombo vya usafiri, na sababu za kimazingira.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya Ajali za Barabarani ya mwaka 2017 zinaonyesha kuwa watu milioni 1.25 hufariki  kwa ajali kila mwaka ambapo watu milioni 20 hadi milioni 50 hubaki na majeraha na ulemavu wa aina mbalimbali. 

Ripoti hiyo inaeleza kuwa nusu ya wanaokufa katika ajali za barabarani zinazotokea duniani kote ni watembea kwa miguu, madereva wa bodaboda na madereva wa magari na kuaathiri asilimia tatu ya pato la ndani la taifa kila mwaka. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW