Air Tanzania, Ethiopian Airlines zinavyopigania soko la India
- Mashirika hayo ya ndege barani Afrika yanafanya kila jitihada za kuingia katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.
- Tayari Air Tanzania limeanza safari zake katika jiji la Mumbai mapema Julai.
- Ethiopian Airlines inazidi kujiimarisha katika nchi hiyo na sasa imetangaza safari mpya katika mji wa Bangaluru.
Dar es Salaam. Siku 13 baada ya Shirika la Ndege la Air Tanzania kuzindua safari za ndege kwenda India, Shirika la Ndege la Ethiopia (Ethiopian Airlines) nalo linakusudia kuanza safari katika mji wa Bangaluru baadaye mwakaka huu ili kuendeleza ushindani wa usafiri wa anga duniani.
Air Tanzania ilianza safari zake Julai 17, 2019 ambapo ndege zake zitakuwa zinaruka moja kwa moja kutoka Dar es Salaam, Tanzania hadi katika jiji la kibiashara na lenye watu wengi la Mumbai la nchi hiyo.
Wakati Air Tanzania ikishikilia soko la Mumbai, Ethiopian Airlines wao wameamua kuingia katika mji wa Bengaluru uliopo katika mkoa wa Karnataka kusini mashariki mwa India.
Katika taarifa yake iliyotolewa leo (Julai 31, 2019), shirika hilo limetangaza kuanza safari za kusafirisha abiria hadi katika mji huo kuanzia Oktoba 27, 2019.
Bengaluru maarufu kama ‘Silicon Valley of India’ unatajwa kama kituo kikuu cha shughuli za teknolojia na ubunifu nchini humo, jambo linalowavutia watu wengi kutoka duniani kufika mahali hapo.
Ethiopian Airlines ni miongoni mwa mashirika makubwa ya ndege barani Afrika. Picha|Jetphotos.
Ikizingatiwa kuwa Ethiopian Airlines ni miongoni mwa mashirika makubwa ya ndege barani Afrika, huenda likajipatia watu wengi kutoka nchi mbalimbali za bara hilo wanaotaka kufika katika mji huo unaokua kwa kasi.
“Ethiopian Airlines ni mdau muhimu katika kuunganisha India na Afrika. Ndege nne mpya za kila wiki zitaunganisha mji muhimu ambao ni kitovu cha teknolojia wa Bengaluru na mtandao wetu unaozidi kupanuka kwa kuongeza ndege mbili za kila siku katika miji ya kibiashara ya Mumbai na New Delhi,” amesema Tewolde GebreMariam, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo katika taarifa hiyo.
Amesema kuongezwa kwa Bangaluru katika mtandao wa shrika hilo nchini India kutatoa fursa kwa wasafiri kutua katika mji wanaoutaka, jambo likalochochea shughuli za biashara, uwekezaji na utalii kati ya India na Afrika.
Kwa sasa, Ethiopian Airlines inasafirisha abiria katika majiji ya Bombay na Delhi na mizigo katika miji ya Bangalore, Ahmedabad, Chennai, Mumbai and New Delhi.
Soma zaidi:
- Waziri azungumzia ndege za ATCL kuchelewa, kuahirisha safari
- Shirika la ndege la Ethiopia limesitisha safari zote za ndege aina ya Boeing 737
- ATCL inavyojitanua kimataifa
Huenda tangazo hilo la Ethiopia Airlines likazidi kuiimarisha Air Tanzania katika kuyafikia masoko ya kimataifa na kuhakikisha inahimili ushindani unaotolewa na mashirika mengine ya ndege duniani.
Air Tanzania Ilikuwa na ndege moja aina ya Bombardier DASH8 Q300 ambayo ilikuwa ikihudumu tangu 2011 kabla ya Serikali kuanza mkakati wa kulifufua shirika hilo lililoanzishwa mwaka 1977.
Kwa sasa Serikali imenunua ndege saba; Bombardier DASH8 Q400 tatu, mbili ambazo zilifika Tanzania Septemba 2016 na moja Juni 2017; Bombardier CS300 mbili na Boeing 787 Dreamliner ambazo zilitua Tanzania kati ya Mei na Julai 2018. Hata hivyo, Serikali imesema ndege nyingine moja itawasili Tanzania mwishoni mwa mwaka huu.
Air Tanzania inamilikiwa asilimia mia moja na Serikali kama ilivyo kwa mashirika ya ndege kama Ethiopia.
Air Tanzania sasa inazidi kujitanua ili kufaidika na soko la kimataifa. Picha|Mtandao.