Ahueni: Serikali ikipendekeza ongezeko la kiwango cha mapato ya waajiriwa
- Imependekeza wafanyakazi wote wenye mapato ya jumla yasiyozidi Sh3,24 milioni kutokuwa na kiwango cha kodi.
- Wafanyakazi wenye mapato ya jumla zaidi ya Sh12 milioni kutozwa asilimia 30 pamoja na kiasi zaidi ya Sh1.5 milioni.
- Lengo la mabadiliko haya ni kutoa unafuu wa kodi ya mapato kwa wafanyakazi.
Dar es Salaam. Serikali inakusudia kufanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Mapato sura 332 yatakayopandisha kiwango cha mapato ya waajiriwa ili kuongeza kiwango cha mapato yasiyotozwa kodi (threshold).
Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango amesema kwa mwaka ujao wa 2020/21 Serikali itaipandisha kiwango cha mapato ya waajiriwa kutoka Sh170,000 hadi Sh270,000 kwa mwezi.
Hiyo ni sawa na kutoka Sh2.1 milioni hadi Sh3.3 milioni kwa mwaka.
“Lengo la mabadiliko haya ni kutoa unafuu wa kodi ya mapato kwa wafanyakazi. Hatua hii pekee inatarajiwa kupunguza mapato kwa Sh517.2 milioni,” amesema Dk Mpango.
Waziri huyo amependekeza kuwa, Mapato ya jumla yasiyozidi Sh3.24 milioni yasiwe na kodi huku mapato ya jumla yanayozidi Sh3.24 milioni lakini hayazidi Sh 6.24milioni kiwango cha kodi kiwe cha asilimia 9.
Zinazohusiana
- Uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 5.5 mwaka 2020
- Yaliyochangia uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 7.2 robo ya pili 2019
- Bidhaa za bia, juisi za unga kutozwa ushuru 2020-21
Pia, kwa wafanyakazi wenye mapato ya jumla yanayozidi Sh6.24.miloni lakini hayazidi Sh9.12 milioni mapendekezo ni tozo ya Sh270,000 pamoja na asilimia 20 kwa kiasi kinachozidi Sh6.24 milioni.
Kwa upande wa wafanyakazi wenye mapato ya jumla yanayozidi Sh9.12 milioni lakini hayazidi Sh12.0 milioni yatozwe kodi kwa kiwango cha Sh846,000 pamoja na asilimia 25 kwa kiasi kinachozidi Sh9.12 milioni.
Na kwa wafanyakazi wenye mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 12.0 milioni yatozwe kodi ya Sh1.566 milioni pamoja na asilimia 30 ya kiasi kinachozidi Sh12,0 milioni.