Ahueni: Kinara wizi wa pikipiki atiwa mbaroni Tanzania

April 20, 2021 11:06 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ametambulika kwa jina la Hamisi Beatus mkazi wa Dar es Salaam  na Ifakara mkoani Morogoro.
  • Alikamatwa atika operesheni maalum ya kupambana na wahalifu vinara wanaojihusisha na wizi wa magari na pikipiki.

Dar es Salaam. Huenda wamiliki wa pikipiki katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro wakapata ahueni na kuishi kwa umani, baada ya kinara wa wizi wa chombo hicho cha usafiri kukamatwa na polisi hivi karibuni. 

Pia Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata baadhi ya wezi wa magari jijini Dar es Salaam. 

Mtuhumiwa huyo ametambulika kwa jina la Hamisi Beatus (27) mkazi wa Manzese jijini hapa na Ifakara mkoani Morogoro ambaye ametajwa kuwa kinara wa shughuli hizo haramu katika mikoa hiyo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema walipomkamata mtuhumiwa alikiri kushiriki shughuli hiyo ambayo imekuwa ikiwaletea watu hasara ya kuibiwa pikipiki zao. 

“Mtuhumiwa huyu alihojiwa na kukiri kuhusika kushiriki kuiba na kupokea pikipiki mbalimbali za wizi kutoka kwa washirika wake waliopo jijini Dar es Salaam na Mkoa wa Morogoro,” amesema Mambosasa mbele ya wanahabari leo Aprili 20, 2021 jijini hapa. 

Beatus alikamatwa katika operesheni maalum ya kupambana na wahalifu wanaojihusisha na wizi wa magari na pikipiki katika jiji la Dar es salaam iliyofanyika katika kipindi cha kuanzia Machi hadi Aprili 2021.


Zinazohusiana:


Kamanda Mambosasa amesema pia wanawashikilia watu wengine 13 kwa tuhuma za kukutwa na magari ya wizi sita likiwemo Suzuki T 387 CKD na Toyota IST (T.627 DJY).

Baadhi ya watuhumiwa hao ni Seleman Seif (52) mkazi wa Toangoma Mbagala na Dickson Kalikila (47), mkazi wa Kyela Mbeya.

Watuhumiwa wote pamoja vielelezo wamekamatwa maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam na mikoa mingine na  wanaendelea kuhojiwa na majalada yatapelekwa ofisi ya Taifa ya mashtaka kwa hatua za kisheria.

Usafiri wa pikipiki wa magurudumu mawili maarufu kama bodaboda umekuwa ni msaada mkubwa wa usafiri katika maeneo mengi yasiyokuwa na usafiri wa uhakika nchini. Mbali na kutoa huduma za usafiri, bodaboda zimetoa ajira kwa vijana wengi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW