Ahueni: Bei za mafuta zaendelea kushuka Tanzania

February 5, 2019 10:40 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Katika lita moja watakayonunua, wateja wa rejareja watapata punguzo la Sh175 kwa petroli, Sh144 kwa dizeli na Sh156 kwa mafuta ya taa kutoka bei ya sasa.
  • Bei hizo zimepungua hadi kufikia Sh2,120 kwa lita moja ya petroli, Sh2,080 kwa dizeli na Sh2,046 kwa mafuta ya taa kwa jijini Dar es Salaam.
  • Bei za mafuta yaliyopitia bandari ya Tanga zitaendelea kuwa zile zile za Januari kwa sababu hakukuwa na shehena mpya.

Dar es Salaam.  Wamiliki wa vyombo vya moto na wananchi watapata ahueni kidogo baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza kushuka kwa bei mpya za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa ikiwa ni mwezi wa pili mfululizo.

Ahueni hiyo inakuja baada ya taarifa ya EWURA iliyotolewa leo kueleza kushuka kwa bei za nishati hiyo kwa bei za rejareja na jumla kuanzia kesho (Februari 6, 2019) kwa mafuta yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam. 

Katika bei hizo mpya, wateja wa rejareja wataokoa Sh175 kwa petroli, Sh144 kwa dizeli na Sh156 kwa mafuta ya taa kwa kila lita moja watakayonunua ikilinganishwa na bei ya sasa.

Bei hizo zimepungua kwa viwango tofauti hadi kufikia Sh2,120 kwa lita moja ya petroli, Sh2,080 kwa dizeli na Sh2,046 kwa mafuta ya taa kwa bei za rejareja jijini Dar es Salaam. 

Hii ina maana kuwa kwa miezi miwili ya Januari na Februari 2019, bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepungua kwa jumla ya Sh316, Sh356 na Sh323 mtawalia.


Soma zaidi: Maumivu:Bei za mafuta zapaa


Hata hivyo, ahueni hiyo haitawagusa wakazi wa mikoa ya Kaskazini kwa kuwa bei za mafuta hazijabadilika kwa sababu Bandari ya Tanga haikuingiza shehena mpya.

Pia bei za mafuta yaliyopitia bandari ya Mtwara zitaendelea kuwa zile zile zilizotangazwa Januari 2 2019, ambapo petroli ilipungua kwa Sh271 na dizeli Sh221 kwa lita.   

Mafuta ni moja ya bidhaa muhimu katika sekta ya viwanda na uchukuzi na ni miongoni mwa bidhaa ambazo hutumia fedha nyingi katika uingizaji wa bidhaa nchini.

Enable Notifications OK No thanks