Ahueni, maumivu: TMA ikitabiri mvua za masika
- Mamlaka ya Hali ya Hewa yatabiri ujio wa mvua za kutosha.
- Mvua zitasidia upatikanaji wa malisho na uzalishaji wa mazao.
- Pia zinaweza kusababisha mafuriko, uharibufu wa miundombinu na kutatiza usafirishaji.
Dar es Salaam. Huenda wakulima na wafugaji wakapata ahueni baada ya kupita katika adha ya ukame kutokana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutabiri uwepo wa mvua za kutosha zitakazoanza kunyesha wiki ya tatu ya mwezi Februari mwaka huu.
Ukame umeripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini baada ya kuwepo kwa upungufu mkubwa wa mvua tangu Oktoba mwaka jana na hivyo kusababisha vifo vya mifugo na kupungua kwa uzalishaji wa mazao shambani.
Hali hiyo iliwaweka katika wakati mgumu wakulima na wafugaji ambao wanategemea mvua kuendesha shughuli zao ili kukidhi mahitaji ya familia.
Hata hivyo, wafugaji na wakulima wanaoishi katika maeneo yanayopata vipindi viwili vya mvua hawataendelea kuathirika na ukame katika maeneo yao kwa sababu mvua zinatarajiwa kuanza kunyesha hivi karibuni.
Msimu wa mvua za masika ni mahususi katika Mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Pia mvua hizo hunyesha katika mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi aliyekuwa akitoa utabiri wa mwelekeo za mvua msimu wa masika za Machi hadi Mei 2022 jijini Dar es Salaam leo Februari 17, 2022 amesema mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
“Ongezeko la mvua linatarajiwa hususan katika kipindi cha mwezi Machi 2022 katika maeneo ya pwani ya kaskazini na mwezi Aprili 2022 kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki,” amesema Dk Kijazi.
Mvua za masika zinatarajiwa kuanza mapema kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Februari 2022 na kuisha mwezi Mei 2022 katika maeneo mengi.
Dk Kijazi ambaye ni Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) amesema pia katika kipindi cha miezi mitatu, matukio ya vipindi vya mvua kubwa zinazoambatana na upepo mkali yanatarajiwa kujitokeza.
Ahueni kwa wakulima na wafugaji
Kwa mujibu wa TMA, unyevunyevu wa udongo na maji ya mvua yatakayovunwa kwa ajili ya umwagiliaji vinatarajiwa kutosheleza mahitaji ya kilimo.
Wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba na kupanda mapema, kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani, mmomonyoko na upotevu wa rutuba, na kuchagua mbegu na mazao sahihi kwa ajili ya msimu huu wa masika, ameeleza Dk Kijazi.
“Wakulima wanahimizwa kufanya palizi kwa wakati, kutafuta na kutumia ushauri wa wataalam wa kilimo katika maeneo yao,” amesema.
Katika msimu wa Masika 2022, malisho na upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo vinatarajiwa kuwa kwenye hali ya kuridhisha katika maeneo mengi nchini.
Hivyo, TMA Inawashawauri wafugaji kutumia mbinu bora za ufugaji kama vile kulisha mifugo kwa mzunguko ili kuhifadhi malisho na kuimarisha uvunaji wa maji ya mvua kwa matumizi ya baadaye.
“Ongezeko la maji katika maziwa, mito na mabwawa linatarajiwa kuchangia kuongezeka kwa chakula na uzalishaji wa samaki,” amesema Dk Kijazi mbele ya wanahabari leo.
Soma zaidi:
- TMA yatahadharisha ujio mvua kubwa
- Watanzania washauriwa kutumia taarifa za hali ya hewa kwenye mipango ya maendeleo
- Ujio mfumo wa taifa wa hali ya hewa kuchochea ujenzi wa viwanda nchini
Maumivu kwa sekta mbalimbali
Licha ya kuwa wakulima na wafugaji watafaidika na ujio wa mvua hizo, pia zinaweza kusababisha madhara katika shughuli zao ikiwemo kuathiri ukuaji wa baadhi ya mazao yasiyohitaji maji mengi, kama vile mahindi na mazao jamii ya mikunde.
Aidha, wanashauriwa kuimarisha miundombinu ya kilimo na kudhibiti visumbufu vya mimea hasa magonjwa ya kuvu ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
TMA inaeleza kuwa magonjwa ya mifugo yanayohusiana na mvua nyingi yanaweza kujitokeza katika msimu huu.
Mamlaka hiyo pia imeonya kutokea kwa matukio ya hali mbaya ya hewa na kuathiri miundombinu ya usafirishaji ikiwa ni pamoja na kuharibika kwa miundombinu ya barabara na reli na ongezeko la ajali barabarani katika usafiri wa nchi kavu.
“Kuchelewa au kusitishwa kwa safari za ndege, mawasiliano hafifu angani na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji katika usafiri wa anga; na ongezeko la ajali kutokana na mawimbi makubwa, uono na mawasiliano hafifu katika usafiri majini,” amesema Dk Kijazi kuwa vinaweza kutokea.
Pia mafuriko, uharibifu wa miundombinu, upotevu wa mali na maisha, milipuko ya magonjwa pamoja na athari nyingine zitokanazo na mvua nyingi zinaweza kujitokeza.
TMA inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, mamlaka za wanyamapori, wasafirishaji, mamlaka za maji na afya kuendelea kutafuta, kupata na kuzingatia ushauri wa wataalam katika sekta husika.
Imefadhiliwa na: WAN-IFRA – Press Freedom. WAN -IFRA haihusiki na maudhui haya.