AfDB yawekeza zaidi Sh5 trilioni miradi ya maendeleo Tanzania

January 25, 2022 7:58 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Fedha hizo ni mikopo na misaada ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
  • Miradi hiyo ikiwemo barabara inalenga kuboresha maisha ya watu.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Lameck Nchemba ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuwekeza Dola za Marekani bilioni 2.47 (Sh5.7 trilioni) katika miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi kiuchumi na kijamii.

Dk Nchemba ametoa shukrani hizo Jijini Dodoma Januari 24, 2022 alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Kipronoh Cheptoo anayesimamia nchi nane za Afrika katika Benki hiyo, ambazo ni Tanzania, Kenya, Ethiopia, Rwanda, Seychelles, Sudan Kusini, Eritrea na Uganda.

Amesema kuwa benki hiyo imeipatia Tanzania mikopo ya masharti nafuu na misaada kwenye miradi 23 ya maendeleo ambapo asilimia 87 ya miradi hiyo iko katika sekta ya miundombinu ikiwemo nishati, barabara, maji na usafi wa mazingira na asilimia iliyobaki imeelekezwa kwenye sekta za kilimo, sekta binafsi na utawala wa kiuchumi.

“Kwa niaba ya Serikali na wananchi, ninapongeza uungaji mkono wa Benki ya Maendeleo ya Afrika katika maendeleo ya nchi kwa kuwa miradi hiyo mikubwa inayotekelezwa kupitia fedha zinazotolewa na benki hiyo zimesaidia kukuza uchumi wa nchi ikiwemo miradi ya barabara ya Ukanda wa Mtwara, Katavi na Tabora,” amesema Dk Nchemba.

Miradi mingine inayofadhiliwa na AfDB kuwa ni kituo cha pamoja cha forodha katika mpaka wa Kenya na Tanzania-Namanga, ambao umesaidia kukuza biashara kati ya nchi hizo mbili pamoja na mradi wa maji na usafi wa mazingira-Arusha, ambao umeboresha maisha ya wananchi wa mkoa huo.

Dk Nchemba aliitaja miradi mingine muhimu ambayo AfDB imetoa fedha ikiwa ni pamoja na mradi wa barabara za mzunguko katika Jiji la Dodoma ambazo amesema zitafungua fursa za kiuchumi wa wananchi wa mkoa huo na mikoa jirani pamoja na mradi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato.


Somo zaidi: AfDB yaipatia Serikali mkopo wa zaidi ya Sh589 bilioni


Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Cheptoo ameipongeza Tanzania kwa umahili wake wa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati inayochangia ukuaji wa uchumi wa nchi na maendeleo ya watu.

Ameahidi kuwa benki yake iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania ambayo ni mshirika ama mwanachama wa benki hiyo kwa kutoa fedha zaidi zitakazosaidia kukamilisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Cheptoo amesema kuwa AfDB itatoa fedha pia kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mipya inayohusu sekta tatu ikiwemo program ya kuendeleza mapinduzi ya viwanda katika kilimo, uendelezaji wa stadi za kazi na ajira kwa vijana pamoja.

Pia itatoa fedha kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Ifakara-Malinyi-Londo hadi Lumecha, uliokusudiwa kuiunganisha mikoa wa Morogoro na Ruvuma kwa ajili ya kukuza fursa za sekta ya kilimo katika maeneo hayo.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV