ACT Wazalendo yampendekeza Luhaga Mpina kuwania Urais wa Tanzania 2025
- Uamuzi huo umefikiwa katika kikao chake maalumu kilichofanyika Agosti 5, 2025.
- Dorothy Semu aliyeteuliwa awali aomba kujitoa ili kupisha chama kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha.
Dar es Salaam. Halmashauri Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo imempendekeza Luhaga Mpina pamoja na Aaron Kalikawe kuwa wagombea wa Urais wa Tanzania kupitia tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Uamuzi huo umetangazwa ikiwa imepita siku moja tu baada ya Mpina ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kisesa na Waziri wa zamani wa Mifugo na Uvuvi kutangazwa kuhamia rasmi chama cha ACT Wazalendo jana Agosti 5, 2025 baada ya jina lake kuachwa katika orodha ya walioteuliwa kugombea ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 6, na Shangwe Ayo, ambaye ni Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Umma uamuzi huo umefikiwa katika kikao chake maalumu kilichofanyika Agosti 5, 2025.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa kwa upande wa urais wa Zanzibar, Halmashauri Kuu ya ACT imependekeza jina la Othman Masoud Othman, ambaye ndiye mwanachama pekee aliyechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo.
Othman pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
“Majina yaliyopendekezwa yatawasilishwa kwa Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho kwa ajili ya kupigiwa kura,” inasomeka taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, Halmashauri Kuu imepokea na kuridhia uamuzi wa aliyekuwa mgombea wa urais wa Tanzania kupitia chama hicho, Dorothy Jonas Semu, kujitoa kugombea nafasi hiyo.
Dorothy ameeleza kuwa amechukua hatua hiyo ili kutekeleza majukumu yake ya kiuongozi na kukiandaa chama kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
Hata hivyo, Mpina atakuwa si mwana CCM wa kwanza kujiunga na upinzani baada ya kukosa fursa ya kugombea nafasi ya uongozi kwenye chama chake.
Mwaka 2020 aliyekuwa kada wa muda mrefu wa CCM na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje Benard Membe alihamia katika chama hicho baada ya kufukuzwa CCM ambapo alitaka kugombea Urais.
Membe hakushinda urais kupitia ACT Wazalendo na alirejea CCM mwaka 2021 ambapo mpaka umauti unamkuta alikuwa mwanachama wa CCM.
Mwaka 2015, Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Edward Lowassa alihamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya jina lake kutopendekezwa kuwania urais kupitia CCM.
Latest



