Urembo wa kucha unavyowaweka matatani wanawake -2
- Kemikali zilizopo kwenye rangi za kucha ndiyo husababisha madhara.
- Licha ya kucha kuharibika, mtu anaweza kupata saratani.
- Wataalam wa afya washauri umakini wakati wa matumizi wa rangi za kucha.
Dar es Salaam. Licha ya kuwa urembo wa kupaka rangi kucha na kubandika kucha bandia kuonyesha madhara kwa baadhi ya wanawake, suala hilo linahitaji jicho la tatu ili watumiaji wapate uelewa na kuwa salama wakati wakitafuta muonekano mzuri wa kucha zao.
Madhara ambayo yameshuhudiwa kwa baadhi ya wanawake ikiwemo kuoza na kubanduka kwa kucha huenda hadi katika viungo vingine vya mwili ikiwemo maumivu ya kichwa na saratani.
Madhara hayo yote yanayoweza kumpata mtu yanatokana na kemikali zilizopo kwenye rangi za kucha na zile kucha bandia.
Kemikali zinazotumika kutengeneza rangi za kucha zipo nyingi na baadhi siyo rafiki kwa kucha za binadamu hasa kama mtumiaji atatumia kwa muda mrefu.
Dk Reinfreed Haule kutoka Hospitali ya Tarime iliyopo Mkoani Mara katika tafiti mbalimbali amesema zipo kemikali tatu za rangi za kucha ambazo zinatajwa ndiyo hatarishi zaidi kwa afya binadamu.
Kemikali hizo kwa lugha ya kiingereza ni ‘Formaldehyde’, ‘Toluene’ na ‘Dibutyl phthalate (DBP)’ ambazo hujikana kama sumu ya kucha (Toxic Trio in nail polish).
“Toluene ina madhara kuanzia harufu yake kwani ipo kama gesi. Mtu akinusa rangi inaingia kwenye mfumo wa neva,” anasema Dk Haule akieleza kazi ya kemikali hiyo ni kuzuia rangi isijichuje.
Zipo rangi za kucha ambazo hazina kemikali hatarishi hata hivyo rangi hizo ni ghali hivyo siowote wanaweza kuzinunua. Picha| Best Products.
Mtaalamu huyo anasema kemikali hiyo inasababisha maumivu ya kichwa mara kwa mara ikiwa mtu atainusa kwa mtoa huduma na anayepakwa rangi.
Pia, kemikali ya Formaldehyde ameitaja kuwa kati ya visababishi vikubwa vya saratani japo inatumika kwenye kucha kufanya rangi ikae muda mrefu na kufanya kucha ziwe ngumu.
“Inasababisha kucha zinaungua zinakua nyeusi, watu wanachanganya na fangasi lakini ukweli siyo huo, ni kucha inakuwa imepoteza rangi wake,” anasema mtaalam huyo.
Kwa upande wa DBP husababisha magonjwa ya ngozi, kuchochea mzio na kucha kuwa kavu.
Madhara huongezeka kwa watu ambao rangi za kucha zao hukaushwa na mwanga maalum (Ultra violent).
Mwanga huo ambao humulikwa ili kukausha rangi ya kucha ili isitoke haraka unaweza kusababisha maumivu ya kucha na saratani kwa mtu endapo utatumika mara kwa mara.
“Kumulikwa mulikwa mara nyingi inasababisha maumivu kwenye viungo na hata kucha kuwasha,” anasema Dk Haule.
Kutokana na kemikali hizo ambazo huenda hazijulikani na watu wanaopenda urembo huo wametakiwa kuchukua tahadhari ili kuziweka afya zao salama.
Rangi za kucha ambazo siyo rafiki kwa matumizi huwa na viungo (ingridients) vitatu ambavyo husababisha madhara ikiwemo kucha kubadilika rangi. Picha| Ella + Milla.
Dk Reinfreed Haule anasema matumizi ya rangi za kucha na kucha za kubandika yana madhara ya kiafya ya muda mfupi na muda mrefu.
Dk Haule anasema kucha kuoza, kubadilika rangi au kubanduka, huo ni mwanzo tu na kwa baadhi wanaowahi, huweza kupata suluhu huku wanaochelewa wakilazimika kubaki na kucha ambazo hawazifurahii.
“Madhara ya matumizi ya rangi za kucha hayaishii kwenye kucha tu kwa baadhi ya wanawake, wameshaathiriwa hadi mifumo ya uzazi kutokana na rangi hizo,” amesema Dk Haule.
Mtaalamu wa kutengeneza kucha kutoka Kitunda mkoani Dar es Salaam, Fahad Amiri anasema ili kujiweka salama dhidi ya madhara hayo, watoa huduma na wanaopenda urembo huo wazingatie taratibu za kupaka rangi.
Anasema muda wa rangi kukaa kwenye kucha hutofautiani kati ya wiki moja hadi mwezi.
Mtaalamu huyo wa masuala ya kucha anashauri kuzipatia kucha muda wa “kuhema” kidogo walau wiki moja, kabla ya kupaka rangi zingine.
Unataka kufahamu ni mambo gani ya kuzingatia kabla na baada ya kupaka rangi kucha zako au kubandika kucha bandia kwenye vidole vyako? Usikose makala inayofuata.
Latest