Maambukizi mapya ya VVU yapungua kwa asilimia 66.1 Tanzania
- Vifo vinavyotokana na maambukizi vimepungua kwa asilimia 82.9.
Dar es Salaam. Tanzania imepunguza maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa asilimia 66.1 ndani ya miaka 15, hatua inayopunguza kasi ya kuongezeka kwa idadi ya watu wanaohitaji huduma za matibabu na uangalizi wa muda mrefu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Profesa Palamagamba Kabudi, aliyekuwa akizungumza Novemba 19, 2026, jijini Dar es Salaam amesema mafanikio hayo ni sehemu ya matokeo ya juhudi za miaka 25 za Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) katika kuratibu mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini.
“Mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2025 ni kupungua kwa maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI kutoka watu 98,754 hadi watu 33,511,” alisema Profesa Kabudi.
Prof Kabudi aliezeza kuwa idadi ya maambukizi mapya imepungua kwa watu 65,243 ikilinganishwa na mwaka 2010, sawa na asilimia 66.1.
Mafanikio mengine yaliyoanishwa na Kabudi ni kupungua kwa vifo vinavyotokana na UKIMWI kutoka watu 5,833 mwaka 2010 hadi watu 25,995 mwaka 2025, ikiwa imepungua kwa asilimia 82.9.
Aidha, kiwango cha maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kimeshuka kutoka asilimia 9.1 hadi asilimia 6.2 katika kipindi hicho, ikiwa imepungua kwa asilimia 31.9 ukilinganisha na kiwango cha awali.
Hata hivyo, hatua hizo ni sehemu ya mafanikio 13 yaliyopatikana katika miaka 25 ya TACAIDS, yakiwemo kuimarika kwa huduma za tiba na matunzo pamoja na upatikanaji wa dawa za ARV bila malipo
Vile vile, kupungua kwa unyanyapaa, kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kuongezeka kwa tohara ya kitabibu kwa wanaume, kuimarika kwa huduma za upimaji wa hiari, upatikanaji wa huduma za kujipima VVU na usambazaji wa kondomu,
Tanzania yavuka malengo ya kimataifa
Sanjari na mafanikio hayo, Tanzania imevuka malengo mawili kati ya matatu ya kimataifa ya 95-95-95, yanayolenga kuhakikisha asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali zao, asilimia 95 ya wanaojua hali zao wanapata dawa za ARV na asilimia 95 ya wanaotumia dawa hizo wanafubaza virusi.
Kulingana na takwimu za mfumo wa DHIS2 hadi Desemba 2025, asilimia 92.7 ya watu wanaoishi na VVU walikuwa wamepima na kujua hali zao, huku asilimia 99.5 ya waliofahamu hali zao wakipata huduma za ARV na asilimia 98.2 ya wanaotumia dawa hizo wakiwa wamefubaza VVU.
Hata hivyo, takwimu hizo zinaonesha kuwa bado kuna pengo la asilimia 2.3 katika lengo la kwanza la 95-95-95, linalohusu kuwafikia watu wanaoishi na VVU ambao bado hawajapima au hawajui hali zao za maambukizi.
Akizungumzia makundi yanayohitaji kupewa kipaumbele katika juhudi za kinga, Profesa Kabudi alisema vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wanachangia asilimia 33.3 ya maambukizi mapya ya VVU, huku asilimia 77.7 ya maambukizi mapya katika kundi hilo yakiwa miongoni mwa vijana wa kike.
Kwa mwaka 2026, maadhimisho hayo yataanza Novemba 24 katika kanda saba nchini na kuhitimishwa Desemba Mosi katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Siku ya UKIMWI Duniani iliasisiwa mwaka 1988 na Shirika la Afya Duniani (WHO), ikiwa ni jukwaa la kuhamasisha mshikamano wa kimataifa katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, kuwakumbuka waliopoteza maisha na kuhimiza hatua zaidi za kuzuia maambukizi mapya.